Na Ibrahim Mkamba
NAOMBA nianze kwa kuwapongeza wasanii wote walioshiriki kwenye shindano la tuzo za Kili Music Awards mwaka huu. Ushiriki wa wasanii hao unaonesha ukomavu wao kisanii kwani walijua kulikuwa kuna kushinda na kushindwa.Kushinda,huongeza hamasa ya jitihada ya kwenda juu zaidi na kushindwa huongeza hamasa ya kufanya jitihada ili safari ijayo ushinde na kwenda juu zaidi.Pongezi za pekee ziwafikie wote walioshinda katika shindano hilo.
Kimsingi,huwa sielewi unakuwepo vipi uwezekano wa baadhi ya wasanii kujitoa kushiriki kwenye shindano hili.Uamuzi huo kisayansi hauwezekani kabisa hata kama wasanii hao wana hoja za msingi sana za kiuchumi na kijamii za kukataa kushirikishwa kwenye shindano hilo.Nitaeleza kwa nini hilo haliwezekani kisayansi lakini naomba nitangulie kuzungumzia kidogo maoni ya baadhi ya walioshuhudia onesho la mwana hip hop Mmarekani mwenye asili ya Jamaica,Sean Kingstone na wasanii wetu kadhaa kwamba Mmarekani huyo alifunikwa na wasanii wetu wa Bongo fleva walipotumbuiza kwenye sherehe ya kuwapongeza walioshinda tuzo za Kili Music Awards za mwaka huu ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee.
Sikuwepo siku hiyo lakini inawezekana kweli gwiji hilo la muziki la kimataifa lilifunikwa na vijana wetu kina Mwana FA,AY,Diamond, Cpwaa,Joh Makini na wengine kama ilivyoelezwa elezwa lakini naamini kufunikwa kwa mwanamuziki huyo mkubwa lakini mwenye umri mdogo, zaidi kulitokana na mazoea kwani kina AT na Stara Thomas, kwa mfano, walipoimba wimbo maarufu wa "Nipigie", wengi wa wabongo waliokuwemo ndani ya Diamond Jubilee walijua hicho ni kitu gani na wengi walikuwa wakifuatisha,bila kukosea hata kidogo,mashairi ya wimbo huo mzuri wanaoujua na kuupenda sana.
Sasa Kingstone akija na ngoma zake ambazo zinajulikana na wachache hapa kwetu,ni wazi wengi tusiozijua tulimuona si lolote lakini tutazithamini sana ngoma hizo zitakapokuja zoeleka masikioni mwetu kwa idadi kubwa.Hii ni kawaida hata kwa bendi zetu za muziki,wanamuziki wetu wa Bongo fleva, Modern Taarab na muziki wa bendi tunayoifahamu toka nje ya nchi. Toka kwao hao wote, nyimbo mpya tupu tusizozifahamu,zinapopigwa au kuimbwa nao kwenye onesho huwa tunaona tumeibiwa hata kama nyimbo hizo ni nzuri vipi.Huwa tunapenda kupata zile tunazozijua ambazo aghalabu huwa tunashiriki kuimba sanjari na wenye nyimbo zao wanapoziimba jukwaani.
Kwa mfano, vijana machachari toka Brazaville,Congo wa Extra Musica wakiwa na "full squad" ya kiongozi na mpiga solo mkali Roga Roga,rapa mahiri Kila Mbongo,mwimbaji mkali Oxy Oxygene,kina Ramatoulaye na wakali wote wa kundi hilo walikuja nchini mwaka 1998 kwa lengo la kutoa heshima kwa nchi hii ya kuzindulia hapa albam yao mpya ya "Etat Major" (E'ta Ma'ja) yenye wimbo huo mkali na kali sana nyingine za "La Pluine","Patinence","Ecart","Cri du Coeur","Racines" na nyingine zilizokuja kuwa maarufu sana hapa kwetu baadaye.
Licha ya umaarufu wa nyimbo hizo wa baadaye na baadhi yake mpaka sasa, siku ya kwanza walipojaribu kuzipiga kwenye uzinduzi wao hapa Dar es Salaam tulizipuuza mno kwani siku hiyo ya uzinduzi wa nyimbo hizo kila walipoanza kupiga wimbo wowote miongoni mwa nyimbo hizo,mashabiki wao wa bongo walipiga kelele kuwataka waache kupiga nyimbo wasizozijua.
Extra Musica walikwama kuzindua albam yao hiyo hapa.Ilibidi watupigie zile tu tulizozijua kama "Losambo","Fred Nelson","Success Extra","Kende",Angela" ,"Inondanation" na nyingine na kuufanya ukumbi wa Diamond Jubelee uchangamke sana.Kama wangekazania hizo za kuzindulia albam na kwa kuwa walishirikiana na Twanga Pepeta ya kina Adolph Mbinga na kina Banza Stone iliyokuwa na wimbo wa "Kisa cha Mpemba" na nyingine nzuri sana, mia kwa mia, tungeona Extra Musica wamefunikwa na Twanga.
Kwa hiyo ni hatari kuwajengea vijana wetu picha kwamba sasa wako juu ya watu kama Sean Kingstone wakati wana mambo mengi ya kujifunza toka kwao.Wakishaingiza imani hiyo vichwani ndiyo kujiona wako kileleni mwa mafanikio na matokeo yake kupotea kama kina Crazy GK,Suma G na wengine.Ndiyo,vijana wetu walikuwa na mengi ya kujifunza toka kwa Kingstone na watu wake kwa shughuli ya jukwaani lakini kubwa zaidi ninaloona walistahili kujifunza ni kila mtu kuthamini muziki wa nchi yake.
Nilisisimkwa mno na habari kwamba watu kadhaa wa kundi la Kingstone walichenguliwa ile mbaya na Taarab kiasi cha kuyarudi mangoma ya Taarab kwa nguvu na kununua baadhi ya CD zake.Unaona,hip hop yetu na R &B yetu kupitia Bongo fleva wala hawakuiona kwani waliiona kama igizo fulani lisilofanikiwa lakini mangoma ya Modern Taarab ya sasa, yasiyo tofauti na Msondo ya enzi ile, yaliwagusa sana.Kwa hiyo wana Bongo fleva wetu tukitaka tufanye biashara ya uhakika ya kimataifa tutumie kupitishia "mistari" yetu kwenye mapigo ya kikwetu kama yale ya Mzee Yussuf ya "Mchum,Issa Kijoti" au ya "Chaja ya Kobe" ya Babu Ayub jambo walilotufundisha kina Kingstone.
Tukirudi kwenye hoja ya msingi,kisayansi kwenye mashindano ambayo mshiriki wake huwa mashindanoni mara tu anaposhiriki kwenye shughuli ya kushindanishwa,hakuna uwezekano wa mtu kujitoa mashindanoni.Njia pekee ya kujitoa ni kutofanya shughuli hiyo kwa kipindi cha kushindanishwa.Kwa mfano,ligi kuu ya soka inapoanza tu inatajwa zawadi ya mfungaji bora.Sasa Mussa Hassan Mgosi, kwa mfano, hawezi kusema kwamba yeye amejitoa kwenye shindano la ufungaji bora wakati ni mchezaji na tena ni mshambuliaji na anacheza kwenye ligi hiyo.
Njia pekee ya yeye kujitoa kwenye shindano la mfungaji bora ni kutochezea klabu yoyote inayoshiriki ligi hiyo.Tena hana haja ya kutuambia kwamba hatashiriki shindano hilo kwani moja kwa moja atakuwa hayumo kama ilivyokuwa kwa watu kama Balozi Dola Sol,Mr Nice,Mandojo na Domokaya,Mabaga Fresh na wengine kwenye tuzo za Kili Awards za mwaka huu kutokana na kutofanya lolote la kimuziki kwenye mwaka huu ulioshindaniwa.
Kisayansi, kama ulifanya kazi ya muziki ndani ya kipindi cha mwaka 2009/2010,moja kwa moja umo shindanoni kwenye kuwania tuzo ya Kili Music Awards,utake usitake kwani tunaweza kuikubali kazi yako hata kama mwenyewe hauko tayari kupambanishwa na wengine.Kushindwa kwani kitu gani? Lazima awepo mshindi hata kama kazi zinazoshindanishwa ni nzuri tupu. Kwa mfano,kwangu binafsi utanipa wakati mgumu kuchagua wimbo bora wa waimbaji walioshirikiana baina ya "Nipigie","Njia Panda" na wimbo mpya unaokuja kasi sana wa "Wrong Number" (wimbo unaoelezea kiufasaha tatizo mojawapo la simu za mkononi miongoni mwa wanandoa).Pamoja na ubora wa kazi zote hizo tatu,zikishindanishwa lazima moja itashinda.Tujenge utamaduni wa kukubali matokea na hivyo kutoogopa kushindana.
Naomba wahusika wa tuzo za Kili Music Awards ifanyieni kazi changamoto yangu ili kila anayeshiriki kwenye masuala ya muziki ajue kuwa moja kwa moja ni mshiriki wa mashindano ya muziki ya kipindi husika kama Jerry Tegete anavyokuwemo kwenye shindano la mfungaji bora hata kabla ligi haijaanza kwa sababu tu yeye ni mshambuliaji na amesajiliwa kucheza kwenye ligi hiyo.Nitashangaa siku John Boko mshambuliaji wa timu ya ligi kuu atakapotangaza kuomba kuenguliwa kwenye shindano la ufungaji bora wa ligi kuu kama baadhi ya wanabongo fleva wetu wanavyofanya kwenye Kili Music Awards wakati muziki wao unasikika hewani mwaka mzima unaoshindaniwa.
Monday, 24 May 2010
Subscribe to:
Posts (Atom)