Saturday, 10 April 2010
TWIGA STARS OYEE,SOKA YA WANAWAKE ZII !
"TWIGA Stars oyee! Oyee! Soka ya wanawake zii! Zii!". Maneno haya ya kihisia ya kushangilia yanaweza kutumika kueleza kwa ufupi hali halisi inayohusu ushindi mkubwa na mzuri wa ugenini wa timu yetu ya taifa ya soka ya wanawake,Twiga Stars wa magoli 3-1 na kisha sare ya muhimu ya 1-1 ya hapa nyumbanii dhidi ya timu kali ya wnawake ya Ethiopia na hivyo kusonga mbele mashindanoni kwa jumla ya magoli 4-2 licha ya kuwepo kwa mwamko mdogo na mbaya wa mchezo wa soka ya wanawake nchini.Ushindi wa timu yetu ya taifa ya wanawake ni "oyee" kwani ni mkubwa na mzuri lakini mwamko wa soka ya wanawake nchini ni "zii" kwani ni mdogo na mbaya!
Naomba nitumie fursa hii kwa kuwapongeza sana wachezaji wetu wote wa Twiga Stars kwa kujitolea kwa nguvu zote kutupa raha Watanzania na kulinda heshima ya Taifa letu.Nawatakia heri na fanaka katika hatua ya mapambano inayofuata dhidi ya Elitrea.Naomba lengo letu liwe siyo tu kufika fainali za mashindano haya nchini Afrika Kusini bali angalau kufika kwenye mechi yenyewe ya fainali kabisa ya fainali hizo na tukifikia hatua hiyo,basi mahesabu yetu yawe kubeba kabisa kombe hilo.
Napenda nitumie fursa hii pia kuwapongeza viongozi wa timu hiyo kina Lina Mhando kwa kupangilia mambo vizuri na kuwezesha mafanikio haya.Pongezi nyingi ziwaendee makocha wa timu hiyo kina Charles "Master" Boniface Mkwasa na Mohammed "Adolf" Rishard kwani kutokana na nitakayozungumza leo hapa chini,kazi yao ni kubwa mno kuwafundisha dada zetu kuliko kuwafundisha watoto wa kiume kwenye mchezo wa soka.
Kutokana na kukosa mfumo uliokamilika wa mchezo huo,ni wazi dada zetu hawa wanakutana na kocha wa uhakika wa mchezo huo ndani ya timu ya Taifa tu na ndiyo maana kina Mkwasa na Adolf wanapaswa wafundishe hata jinsi ya kutuliza mpira na jinsi ya kupiga mpira wa kutoa pasi na kadhalika kama nilivyowahi kumuona kwenye picha ya gazetini Adolf akimfundisha dada yetu mmoja wa Twiga Stars jinsi ya kupiga mpira wa lengo fulani.Hongera sana kwa wadau wote waliofanikisha ushindi wa Twiga Stars.
Si mara chache kwenye safu hii nimekuwa nikihoji kuhusu mipango yetu mingi isiyo mizuri ya michezo na ninasikitika safari hii tena nitafanya hivyo kuhusu mipango isyo mizuri ya maendeleo ya soka yetu ya wanawake ambayo kwa sasa ina hadhi kubwa dunia nzima.Naomba nirudie tena na tena na labda kuna siku nitaeleweka kwamba soka ya vijana wa chini ya miaka 20,17 na chini ya hapo itatengenezwa tu na serikali yenyewe na wala si klabu za soka.Kusema kuwa klabu inaweza kutengeneza timu ya watoto wa chini ya miaka 17 ni uongo dhahiri na hata anayeelekeza hivyo anajua kuwa hilo haliwezekani.
Nahoji kama nilivyotangulia mara kadhaa kuhoji kuwa utamuwekaje mtoto wa miaka 15,16 au 17 katika maisha ya soka ya wakati wote wakati mtoto huyo anapaswa awe shuleni sekondari wakati huo huku elimu yetu ya msingi sasa ikiwa mpaka kidato cha nne? Kwa hoja hiyo,ninasisitiza tena kuwa soka ya vijana ya uhakika haitakuwepo nchini mpaka serikali itakapoanzisha shule bora zilizokamilika kivifaa vya kufundishia za michezo za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha sita kwa kila kanda ambamo watoto wetu wenye vipaji vya michezo,ikiwemo soka ya wanaume na wanawake, watasoma humo wakifundishwa na waalimu bora wa masomo yote pamoja na waalimu bora wa michezo. Shule hizo zitakuwa ndizo timu za uhakika za watoto wa umri wa chini ya miaka 17 na 20 wa kiume na kike ikizingatiwa kuwa hakuna mtoto wa kuishia darasa la saba sasa kwani, kama nilivyotangulia kusema,elimu ya msingi sasa ni ya kidato cha nne.Vinginevyo,ni usanii mtupu kutengeneza timu ya uhakika ya watoto.
Ni katika muktadha huo,naona ipo haja pia kwa serikali kuweka mkono katika maendeleo ya soka ya wanawake. Tuna timu nzuri ya soka ya taifa ya wanawake lakini tuna klabu ngapi nchini za soka za wanawake? Hizo chache ziko wapi nchini? Sumbawanga kuna ngapi? Maswa ziko ngapi? Je kuna timu hizo Kibondo na Mahenge? Je si kweli kwamba kote huko kuna timu za soka za wanaume? Je si kweli kwamba hata huko wako wanawake wanaopenda na wanaoweza kucheza soka lakini hawajafunguliwa mlango wa kuingia ndani na kuucheza mchezo huo?
Bila kuwa na klabu za kutosha za soka ya wanawake,tunategemea timu hii ya taifa inayoundwa na kina Esther Chabruma kwa miaka kadhaa sasa itaendeleaje kuwa na uimara ule ule kwa miaka kadhaa ijayo? Kwa msingi huo,ni ushauri wangu kuwa serikali yetu ifanye yafuatayo:- Kwanza,ihakikishe inarudisha haraka sana michezo mashuleni na hivyo kurudisha mashindano ya UMISSETA.Na katika kufanya hivyo,ielekezwe kuwa michezo hiyo mashuleni ijumuishe soka ya wanawake.Katika utekelezaji mzuri wa hilo,ni vizuri ikaundwa wizara ya kisekta itakayojumuisha wizara zinazohusika na michezo na elimu.Pili,serikali itengeneze nyaraka za maagizo kwa ofisi zake za mikoa zenye maafisa utamaduni na michezo za kuweka mkakati wa kiserikali wa kuanzishwa na/au kuimarishwa kwa soka ya wanawake kwenye wilaya zote nchini.
Kwa hilo,serikali kuu inapaswa itoe mwongozo tu wa nini kifanyike huku kila mkoa ukipimwa kwa ubunifu wake wa kufanikisha vizuri suala hilo kama ni kupitia kwa wafanya biashara wakubwa wapenda soka wa maeneo husika,kama ni kwa taasisi za umma zilizopo kwenye maeneo husika na kwa njia yoyote halali ya kufanikisha jambo hilo la kheri. Kwa mpango huo,baada ya muda kutakuwa na ligi za kusisimua za kitaifa za soka ya wanawake,kutakuwa pia na Taifa cup ya soka ya wanawake na tutakuwa na timu ya taifa imara ya soka ya wanawake kwa nyakati zote.Sifa mojawapo ya uongozi bora ni ubunifu kama aliokuwa nao hayati Dr.Kleruu kwenye maendeleo ya kilimo,hayati Dr.Lawrence Gama kwenye maendeleo ya michezo na hayati Edward Sokoine kwenye usimamizi makini na madhubuti wa utekelezaji wa kazi ya umma.
Hebu maafisa utamaduni na michezo wa mikoa wapewe kazi.Kwenye u-Dar es Salaam huu wa ligi kuu yetu,kwenye hali hii ya soka yetu kuendeshwa kwa njia huria na kwenye kufa kabisa huku kwa ngoma zetu za asili ambazo mtu akijihusisha nazo sasa anaonekana amepitwa na wakati,mshamba,mchafu na hakusoma, maafisa utamaduni na michezo wa mikoa na wilaya wana kazi gani! Wapewe kazi ya kuratibu uanzishwaji na uimarishwaji wa soka ya wanawake mikoani.
Faida ya kuimarika kwa soka ya wanawake nchini si ya kimichezo tu bali pia ya kijamii na kiafaya.Wasichana watakaojihusisha na mchezo huo wataondoka kabisa katika kufanya mambo yasiyokubalika na jamii ikiwemo kujihusisha na ngono zembe na kuupata ugonjwa wa UKIMWI.Kwa hiyo utaratibu huo utalifanyia taifa jambo kubwa lililojificha kuliko tunaloliangalia na kuliona kwa macho.
Naomba kuwasilisha maoni yangu kwa utekelezaji ili kesho na kesho kutwa tuseme; "Twiga Stars oyee, oyee.Soka ya wanawake oyee,oyeeee!
MWISHO
0713 297085 na 0786 297085
Friday, 9 April 2010
TAALUMA NYINGI NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA MICHEZO NA SANAA
- Hisabati
Wataalam wa hisabati ni mwisho wa matatizo yote katika kupangilia mambo yoyote ya kimaendeleo ila kwa bahati mbaya sana jamii nyingi haziujui ukweli huo na hivyo kutowatumia wataalam hawa, wenye taaluma isiyo ya kawaida, katika kupanga mipango sahihi ya maendeleo.Hawa wana ujuzi wa kukuambia kwamba kama unahitaji kufanikiwa katika jambo fulani unapaswa uanze na nini mpaka wakati gani,halafu simamisha hiki kwa muda huu na anzisha hiki.Hiki cha pili kikifikia hatua hii,anza kutekeleza kile cha kwanza pamoja na hiki.Viwili hivi vikifikia hatua hii,simamisha kabisa na anza lile kubwa lao ambalo likifikia hatua hii,yale mawili yaunganishwe nalo na hapo utapata mafanikio haya na haya.
Wataalam hawa wakitumika vizuri,watashauri kwa usahihi sana mipango yetu ya soka, kwa mfano, ipangiliwe pangiliwe vipi kwa kuhusisha shule za soka,soka ya vijana,soka ya kulipwa nje ya nchi,uwepo wa walimu bora wa soka,uwepo wa ligi madhubuti za soka,uwepo wa viongozi makini wa soka na uwepo wa kanuni nzuri na za kutekelezeka za soka.Kipi kitangulizwe na kiende mpaka wapi ndipo kianze kingine na vipi viende kwa pamoja na kwa muda gani kabla ya tathmini ya kwanza.Watu wa hisabati tu ndiyo wanaweza kukupangia kisayansi mambo hayo kwa kutafuta maendeleo. Tuwatumie hivyo baadhi yao badala ya wote kuwaacha kuwa waalimu wa vyuo vya elimu ya juu tu.
- Mawasiliano (Information Technology)
Watu wa taaluma hii ndiyo watunzaji wa uhakika, kwa njia ya elektroniki, wa kumbukumbu zote za mipango yote ya kimichezo ambapo siku za usoni ukitaka kujua kiliazimiwa nini cha kimichezo na kingepatikana kwa njia ipi,hawa jamaa watakupa kumbukumbu zote hizo.Mtu atasema kuwa hilo linaweza kufanywa na mtu wa taaluma yoyote ile.Hapana.Kwanza,hata kama linaweza kufanywa na mtu wa taaluma yoyote,lakini wa taaluma hii atalifanya kwa uhakika zaidi.Pili,jamaa hawa wana uwezo wa kutengeneza programu mbalimbali za kompyuta, rasmi kwa kufanikisha mipango kadhaa mizuri ya kimichezo,jambo ambalo mtu asiye wa taaluma hii haliwezi.Wasiachwe pembeni wataalam hawa kwenye mipango yetu ya maendeleo ya michezo.
- Sayansi
Mwanasayansi per se ni muhimu sana katika maendeleo yetu ya michezo kwani ni yeye ndiye atakayeshauri aina ya vyakula vya wachezaji na viliwe kwa mpangilio gani kutegemeana na aina ya michezo. Ni yeye atakayeshauri saa za wachezaji kulala. Kwa ujumla wote ataaangalia mambo yote ya kiafya ya wachezaji kabla hawajaumia au kuumwa. Ni muhimu sana wanataaluma hii kutumika katika kutafuta maendeleo yetu ya michezo.
- Udaktari
Umuhimu wa wanataaluma wa taaluma hii kwenye maendeleo ya michezo hauhitaji maelezo marefu kwani kila mtu wa michezo anaufahamu. Wao huangalia afya za wachezaji wanapoumia au kuumwa. Mchezaji majeruhi hachezi bila daktari kuthibitisha kwamba anaweza kufanya hivyo.Wana umuhimu mkubwa mno madaktari kwenye michezo yote.
- Ualimu
Ni kosa kubwa kuwaacha nje wenye taaluma ya ualimu katika maendeleo ya michezo.Kwa jinsi taaluma yao ilivyo,waalimu ni walezi na wanasaikolojia.Ukiwaweka nje wanataaluma hawa, ni wazi utaweza kusababisha baadhi ya wanamichezo kuuchukia na kuuacha mchezo walio na kipaji nao kikubwa kwa sababu ya kero fulani fulani zinazowasababisha wafanye mambo ya kuwafanya waonekane washenzi mbele ya wenzao kwenye timu.Wasio na taaluma ya ualimu,huwatimua wachezaji hao kwamba hawana nidhamu lakini kumbe wangewekwa kwanza mikononi mwa walezi wenye uelewa wa saikolojia,matatizo yao yangebainika na wangewekwa kwenye mstari mzuri kimaadili na kuendelea kutesa sana kwenye michezo kwa faida yao na ya taifa lao. Walimu ni muhimu sana kwenye maendeleo ya michezo.
- Uhandisi
Hakuna maendeleo ya michezo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa shule maalum za michezo,viwanja rasmi vya michezo na miundombinu ya kufikia kwenye shule hizo na viwanja hivyo. Ni wenye taaluma ya uhandisi wa ujenzi (civil engineering) tu ndiyo wenye uwezo wa kushauri kuhusu vitu hivyo vya muhimu.Yaani shule ya michezo iwe na vitu gani na wao ndiyo wanaojua viwanja rasmi vya michezo mbalimbali viweje.Wahandisi wasiachwe nje kwenye maendeleo ya michezo.
- Uanasheria
Nemo judex in causa sua, delegatus non potest delegare,in pari delicto portior est conditio defendentis,audi alteram partem,actus non facit reum nisi mens sit rea. Hii ni misemo michache ya kilatini inayotumika sana katika shughuli za kisheria.Msemo wa kwanza unamaanisha "mtu hapaswi kuwa jaji kwenye kesi inayomhusu".Msemo wa pili unamaanisha "aliyekaimishwa madaraka hapaswi kuyakaimisha kwa mwingine".Unaofuatia unamaanisha "kwenye utata kiushahidi,utata huo lazima umnufaishe aliyeshtakiwa".Halafu ule mwingine una maana "sikiliza pande zote kwenye kesi" na wa mwisho unamaanisha "kitendo hakimfanyi mtu kuwa mhalifu wa kosa kama hakuwa na nia ya kutenda kosa hilo".
Misemo hiyo inaonyesha jinsi taaluma ya sheria ilivyojaa busara tele na mantiki kibao! Wenye taaluma hii ni muhimu sana kwenye maendeleo yetu ya michezo kwani ni wao ambao watatengeneza kanuni zenye mantiki na za kutekelezeka na ni wao ambao watakuwa washauri wazuri katika kuepuka kufanya mambo ya kutuletea hasara kikanuni. Ni wachambuzi wazuri wa mambo mbalimbali ya kimaisha.Ni muhimu sana kuwajumuisha kwenye mikakati ya maendeleo kimichezo.
- Uchumi
Ikizingatiwa kuwa michezo inaweza kuingiza pesa na kuwatajirisha wahusika fulani wa michezo hiyo kama klabu za soka na chama cha soka cha nchi,watu wenye taaluma ya uchumi ni muhimu sana katika mipango yetu ya maendeleo ya michezo.Ni muhimu sana kwao kujumuishwa kwenye mipango yetu.
Huu ndiyo mchango wa taaluma tofauti katika maendeleo yetu ya michezo.Tunapopanga chochote cha kimaendeleo kimichezo,tufikirie haja ya kuwajumuisha wenye taaluma tofauti kama ilivyoelezwa hapa.Mara nyingine tutaangalia mchango wa taaluma tofauti kwenye sanaa.
Tuesday, 6 April 2010
MICHEZO NA SANAA NI SUALA LA KIMFUMO
Shughuli zote hizi hazihitaji kusimamiwa na wanasiasa bali zinahitaji kuwa chini ya watendaji wakuu waliobobea kiutaaalam na kiuzoefu kwenye shughuli hizo na watakaopata ajira zao kwa michakato sahihi na si uteuzi ambapo wakivurunda, watawajibishwa katika taratibu za kawaida za ajira. Kiutendaji,hao watawajibika moja kwa moja kwa Rais,Makamu wake au Waziri Mkuu,kutegemeana na mgawanyo wa kazi za wakuu hao watatu wa nchi.Hapo itakuwa ni kazi sana,unafiki au kukomoana hakuna na matokeo yake ni maendeleo tu kwa kwenda mbele!
Monday, 5 April 2010
KARIBUNI WANAMICHEZO NA WASANII KWENYE www.spotisana.com
www.spotisana.com ni mtandao mpya utakaokuwa unajihusisha na mijadala mizito na yenye mantiki ya michezo na sanaa. Michezo ("spoti") itahusisha michezo yote ikiwemo ya jadi kwa kuijadili kwa hoja kutokana na kuwepo kwa jambo zito la kujadilika kuhusu michezo hiyo. Si suala la kutaja tu na kuzungumza vitu vyepesi vyepesi kuhusu michezo hiyo bali ni kujadili kwa hoja juu ya uendeshaji wake,usimamizi wake,kanuni zake na uhalali,utekelezekaji na umantiki wa kuwepo kwa kanuni hizo,mipango thabiti ya maendeleo ya michezo hiyo, maisha ya wachezaji na yote mengine ya uzito huo.
www.spotisana.com itathamini hoja ya kila mchangiaji wa michezo hata kama itakuwa imetolewa kwa misingi ya ushabiki wa Yanga au Simba lakini jambo la msingi hoja hiyo iwe ya kujadilika na iwe na mantiki.Tusiogope kuonyesha ushabiki wetu kama mimi ambavyo siogopi.Ukipanda kwenye gari langu dogo binafsi la kutembelea,utaona ushahidi wa wazi kwamba mimi ni shabiki wa Simba kwani kumebandikwa kitu kinachoeleza hivyo.Ukifika ofisini kwangu ndani ya jiji la Dar es Salaam,Tanzania, utaona ushahidi wa wazi kwamba mimi ni shabiki wa Yanga kwani kuna ushahidi mkubwa na wa wazi wa kuthibitisha ukweli huo.Nazipenda zote na kuzitendea haki zote siku zote.
Mtandao huu utahusika pia na sanaa inayojumuisha filamu,maigizo,vichekesho,muziki wa aina zote unaotengenezwa Tanzania,ulimbwende,lugha na yote kabisa ya kisanii.Jina "spotisana" linaweza kutafsirika kwa usahihi kabisa kama "spoti kwa kwenda mbele" au "spoti ile mbaya" ama "spoti mwanzo-mwisho" lakini maana iliyo rasmi zaidi ni "spoti na sanaa".Kiunganishi "na" kimeondolewa na hivyo jina lingebaki kuwa "spotisanaa" ambapo kwa kutoelewa,watu wangeohoji "a" ya mwisho ilikuwa na umuhimu gani kuwepo. Kwa kuwaondolea utata huo,tukabakisha neno linaloweza kutafsiriwa kama "spoti mno" au "spoti kwa wingi" lakini ukweli ni kwamba www.spotisana.com inamaanisha "michezo na sanaa".
Lugha zitakazotumika hapa ni Kiswahili na Kiingereza ambapo Kiswahili kitakuwa na nafasi kubwa zaidi ikizingatiwa kuwa mtandao huu ni wa Watanzania ambao kwa wengi Kiswahili ni lugha yao ya kwanza na karibu kwa wote ni lugha ya kuzungumzwa kila siku angalau kidogo kwa wenzetu wanaoishi ughaibuni.
- Wanamichezo na wasanii
Kwa tafsiri ya mtandao huu,wanamichezo na wasanii ni wale wote wanaojihusisha na nyanja hizo kama wachezaji na wasanii mbalimbali,walimu wa nyanja hizo,viongozi,wanaojihusisha kuandika au kutangaza kuhusu nyanja hizo,wawezeshaji wote wengine na wanaozijua na kuzipenda ingawa hawashiriki. Kwetu,wote hao ni wanamichezo na wasanii na kamwe wale wanaozipenda na kuzijua tu fani hizo wasicheze mbali na mtandao huu kwani kwetu,hao pia ni wanamichezo na wasanii.
Baada ya kueleza hayo,kwa moyo mkunjufu kabisa naomba niwakaribishe kwa furaha tele kwenye www.spotisana.com .Karibuni sana Watanzania wote popote mlipo Ulimwenguni.
Ibrahim Jaffar Mkamba.