Search This Blog

Thursday, 15 April 2010

NAPENDA SANA IRUDI TANZANIA ILEEE....

Na Ibrahim Mkamba

KWA kweli mwenzenu sina uwezo tu.Lakini ningekuwa na uwezo ningeirudisha Tanzania ilee ambayo wananchi wake waliipenda kwa dhati.Napenda sana irudi Tanzania ilee ambapo kiongozi mkuu wa nchi kama Rais Julius Kambarage Nyerere,Makamu wake wa kwanza Abeid Amani Karume na Makamu wake wa pili Rashidi Mfaume Kawawa, walipotembelea mahali,wananchi walikuwa na furaha isiyo na kifani ya kuwaona viongozi hao.Ilikuwa furaha ya dhati na iliyopitiliza.

Napenda sana irudi Tanzania ilee iliyojaa nyimbo nzuri za kuisifu na kuwasifu viongozi wake ukiachilia mbali wimbo wa Taifa uliokuwa unaheshimika sana kama ilivyokuwa ikiheshimika sana bendera ya Taifa.Napenda sana irudi Tanzania ile ambayo sisi wanafunzi wa shule za msingi za wakati huo nchi nzima tuliimba vizuri na kwa moyo wa furaha nyimbo kama "Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote,nchi yangu Tanzania jina lako ni tamu sana...","Tazama ramani utaona nchi nzuri,yenye mito na mabonde mengi ya nafaka...","Sisi tunataka kuwasha mwenge,tunataka kuwashaa mweenge na kuuweka juu ya mlima,mlima Kilimanjaro..." na nyingine nyingi ambazo sijui zilikuwa zikitungwa na kina nani!

Napenda sana irudi Tanzania ilee ambayo ilijaa bendi za shule za brass band kwa shule zote ambapo bendi hizo zilileta msisimko mkubwa na uchangamfu wa hali ya juu kwenye maeneo ya shule hizo.Aidha,bendi hizo ziliwajenga wanafunzi kiakili na moyo wa kupenda shule,ziliimarisha uzalendo wa wanafunzi kupitia nyimbo zake na zaidi ya yote zilitengeneza wanamuziki wengi wa miaka iliyofuata.

Muziki wa bendi hizo ulitumika kwa ukaguzi wa usafi asubuhi ambapo wimbo wa "baba paka alisema" toka kwenye hadithi ya kitabu cha watoto wa madarasa ya chini cha kujisomea ulikuwa maarufu zaidi kwa shughuli hiyo huku nyimbo kadhaa za siasa zikitumika pia kama "Tumsifu Mheshimiwa,Julius aee,Kambarage aee,Nyerere...".

Aidha,muziki wa bendi hizo ulitumika kuongoza gwaride la kuzunguka kidogo eneo la shule kabla ya kila darasa kujigawa kuingia darasani kwake.Katika gwaride hilo,ziliimbwa nyimbo za burudani tu kama "Rabeka wanisumbua" kutoka kwa mwanamuziki wa Kenya pamoja na nyimbo za kuelimisha kama "Tuna maadui wetu watatu,kwanza ujinga,pili magonjwa,tatu umasikini watukondesha..." pamoja na nyimbo za siasa kama "Nyerere yupo,Nyerere yupo,ukiona kundi la siasa Nyerere yupo..." ambapo kwenye beti nyingine walitajwa Karume na Kawawa.

Bendi hizo za shule zilikuwa burudani tosha si kwa sare zake nadhifu za wanabendi tu,wala si kwa midundo yake ya ngoma ndogo tu zinazovaliwa kiunoni kwa pembeni wala si kwa ngoma kubwa tu inayovaliwa tumboni na kudundwa itoe mlio kama besi gitaa na wala si kwa filimbi tu zinazopangiliwa sauti kama matarumbeta ya bendi za muziki yanavyopangiliwa na wala si kwa band master tu anayeongoza bendi akiwa na fimbo yake iliyoitwa hockey (hoki) iliyokuwa inapambwa kwa rangi kadhaa na usinga kidogo ambayo kiongozi huyo alikuwa akiichezea kwa madaha kama kuizungusha,kuirusha juu na kuidaka kisha kuipitisha kati ya miguu na kuiridisha mbele na vimbwanga vingine.

Ni muungano wa yote hayo ndiyo uliokamilisha uzuri wa burudani hiyo ya kipekee ambayo tuliifaidi sana ndani ya Tanzania ilee.Kila mmoja aliipenda sana burudani hiyo wakati huo kwani bendi ikipita mitaani,hata watu wazima walitoka nje ya nyumba zao kuitazama huku kila mtu akivutiwa zaidi na "idara" tofauti zilizotajwa hapo juu za bendi hizo.

Napenda sana irudi Tanzania ilee ambapo wanafunzi wa shule za msingi walikimbia mchakamchaka asubuhi.Mchakamchaka huo uliwaimarisha kiafya ya mwili na akili huku wakijifunza mengi ya kitaifa kama maadui wa nchi yetu,siasa ya nchi yetu na kadhalika katika kujenga uzalendo wao kwa nchi yao kupitia nyimbo nyingi za mchakamchaka zilizojumuisha pia nyimbo za burudani tu za kuwafanya wasijisikie uchovu kama "kipande cha papa ugali wa muhogo kula..." na nyingine za aina hiyo.

Napenda sana irudi Tanzania ile iliyochangamka sana tofauti na hii iliyo nyoronyoro.Naipenda Tanzania ile kwani ilikuwa na vikundi vya hali ya juu vya kwaya toka kile cha Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU,TANU Youth League (TYL), cha mzee Makongoro hadi vya shule zote za msingi Tanzania vilivyokuja kuongozwa kiumaarufu na kikundi cha kwaya cha Shule ya Msingi Uponera Mahenge,Ulanga,Morogoro chini ya Mwalimu mahiri wa shughuli hiyo,Amani Mkolokoti Itatiro.

Aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Ndugu Aboud Jumbe,ambaye kwenye uongozi wake katika nafasi hiyo aliitembelea Tanzania nzima,alipouona umahiri wa kikundi hicho akiwa ziarani Mahenge,alikialika kwenda Zanzibar na kilifanya hivyo.Nyimbo za kwaya enzi hizo zilikuwa zikitungwa kirahisi mno.Fikiria kulipokuwa na kazi isiyo ya jasho toka wimbo "TANU yajaenge nchi" kwenda "Chama chetu cha Mapinduzi,chajenga nchi".Leo kuna chama gani kina wimbo miongoni mwa CUF,CHADEMA na NCCR Mageuzi,nikitaja vichache vya upinzani?

Hebu kwa mzee mwenzangu kumbuka mashairi mazito ya wimbo wenye maneno; "Chama chetu kimetuongoza hadi uhuru tulipoupata,kinaendelea kuongoza kufikia lengo ujamaa,Mwenyekiti Mwalimu Nyerere,mwenye hekima na wingi wa sifa Tanzania...".Hebu kumbuka CCM ilivyozaliwa na nyimbo nyingi nzuri za kwaya kama "Kuzaliwa kwa chama kipya,tarehe tano mwezi wa pili sabini na saba,ewe Mungu kipe baraka..." na ule uliokuwa unatumika kuanzia na kumalizia kipindi cha RTD cha "Ujumba wa Leo" pamoja na nyingi nyingine.Sijui waliotunga nyimbo hizo wako wapi leo.

Napenda sana irudi Tanzania ilee ambapo tulikuwa tukiburudika sana na ngoma zetu nyingi za asili za makabila yote kama Mkwajungoma,Mdundiko,Gombesugu,Tokomile,Libanta,Sangula madela,Sindimba,Mbeta,Silanga,Kayamba,Mdumange,Lizombe,Mng'anda,Hiari ya Moyo nikitaja chache sana toka makabila machache sana miongoni mwa nyingi sana toka makabila mengi sana ya Tanzania.

Ngoma hizi zilifanya sherehe mbalimbali za kitaifa na za kidini kufana mno kwani uwanja mmoja mkubwa uliweza kuwa na ngoma kadhaa ambapo watazamaji,wakiwa na nguo zao nadhifu na pilau tumboni,walikuwa wanahama toka ngoma hii hadi nyingine na kuganda mahali kutegemea vimbwanga vya ngoma hiyo.Leo hii ngoma hizo,ambazo zote miongoni mwa zinazochezwa kwa mduara zinakwenda kinyume cha mwendo wa mshale wa saa, ziko wapi? Tanzania gani hii!

Napenda sana irudi Tanzania ilee iliyojaa uchangamfu mkubwa kwa vijana kupitia hot funky na slow funky kwenye kumbi nyingi za disco kama Mbowe (sasa Club Billicanas),YMCA,Silversands,Motel Villa De Tanzanie,Bahari Beach na nyingi nyingi nyingi Tanzania nzima.Madisco hayo yalikuwa chini ya ma-DJ maarufu waliojaa ufahamu mkubwa wa muziki na uchangamfu wa hali ya juu.Ndani ya kumbi hizo,manukato,moshi moshi,mapovu mapovu na mataa ya kubadilika badilika uwakaji yaliyokuwa yakibadili badili rangi za nguo na hata uchezaji kimuonekano ziliifanya Tanzania ile iwe ya kipekee kabisa tofauti na hii isiyo na disco la vijana wa sasa na kubakiza walewale waliocheza madisco hayo lakini sasa wakiwa kwenye madisco ya bakulutu yasiyo na vimbwanga kama taa taa.

Napenda sana irudi Tanzania ilee iliyojaa kumbi za sinema kama Avalon,Empire,Empress,Cameo,Odeon,Starlight na Drive In kwa Dar es Salaam ambapo kila mji mkuu wa mkoa ulikuwa na jumba moja.Nani kasema mkiwa na uwezo wa kuangalia sinema nyumbani majumba ya sinema si muhimu? Mmesahau au hamfahamu kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu (Kiongozi wa juu zaidi) wa Norway,Olof Palme,aliuawa mwaka 1986 akitoka kuangalia filamu kwenye jumba la sinema? Kwani yeye kama kiongozi namba moja wa nchi alishindwa nini kuwa na filamu yoyote nyumbani kwake?

Hamjasikia kwamba Rais Barrack Obama wa Marekani anapenda sana kwenda kuangalia filamu kwenye majumba ya sinema na familia yake? Kwani hawezi kuwa na filamu zozote azitakazo kwa kuziangalia akiwa nyumbani kwake? Majumba ya sinema ni sehemu ambayo iko si kwa kuangalia picha tu bali kwa kujumuika,kubadilishana mawazo na kufanyia matembezi.Hii ndiyo sababu waliotangulia kuwa na video sets miaka zaidi ya 100 kabla yetu mpaka leo wana majumba ya sinema yanayofanya biashara nzuri tu.

Napenda sana irudi Tanzania ilee iliyokuwa na Jeshi kamili la Kujenga Taifa na vijana wote toka shuleni na taasisi za elimu walipitia huko kwa mujibu wa sheria.Walijengwa mno kiu-sharp wa kukabili hali yoyote ile,kiukakamavu, kujua silaha na jinsi ya kuzitumia.

Napenda sana irudi Tanzania ilee ambapo kulikuwa na bendi nyingi za muziki wa dansi toka kona zote kama Highland Jazz ya Iringa,Dodoma International ya Dodoma,Matimila Band ya Songea,Mitonga Jazz ya Lindi,Kiko Kids,Tabora Jazz na Nyanyembe Jazz za Tabora,Lake Jazz ya Kigoma,Mara Jazz,Wana Sensela ya Musoma,Usalama Jazz ya Moshi,Kurugenzi Jazz ya Arusha,Atomic,Jamhuri na Amboni Jazz za Tanga,Zanzibar Jazz ya Zanzibar na bendi kibao za Dar es Salaam. Nimetaja bendi hizo kuonyesha jinsi kanda zote za nchi yetu zilivyokuwa na bendi za muziki.Ndiyo maana hapo sikuzitaja bendi kibao za Mkoa wa Morogoro kama Moro Jazz,Cuban Marimba,Kilombero Jazz,Kwiro Jazz,Kilosa Jazz,Tumbi International na Mzinga Troupe.

Bendi zote nyingi zilizoishi katika vipindi tofauti zilitunga nyimbo nzuri mno,zenye ujumbe wa maana za kueleza mambo tofauti tofauti huku vyombo vikipigwa kwa ufundi mkubwa.Tanzania ile ilikuwa na wapigaji wengi wengi wengi mno wa vyombo vyote tofauti tofauti vya muziki.Wanamuziki wa wakati huo waliimba nyimbo katika hisia zilizolingana na ujumbe wa nyimbo hizo.Angalia mifano hii:-"...kukupenda sana nimejichongea na ambapo hiyo ndiyo kawaida kuseema kweli unajidanganya...."(Muhidina wangu,Western Jazz,mwaka 1971)."....wananchi sote tusikubali,kuingiliwa na adui nchini,sasa ni wakati wa mapinduzi,kila mwananchi ajue silaha..."(Polisi Jazz,mwaka 1971).

Wakati wimbo ule wa Western Jazz,Wana saboso,uliimbwa kwa kunung'unika kwa sababu ulikuwa wa kulalamika,ule wa Polisi Jazz,Wana sombrelo,uliimbwa kwa kuhamasisha kwani ulikuwa wa kuhamasisha.Angalia tena mifano hii:-...fanya subira kidogo,binti utakua, fanya subira kidogo mwali wetu utakua,hapo ndipo uweze maisha ya kuchagua,lakini kama wazazi yalo bora tunasema,maisha ya utuliivu ni maisha ya kufuata,tunakukanya mapema isitufike aibu ee..."(Maneno haya yameimbwa na Zahir Ally,kwenye wimbo wake "Mkanyeni huyo Binti" akiwa na Kimulimuli Jazz,wimbo uliorekodiwa mwaka 1978)

"...ugomvi wetu ulopita ni kuoa mke wa pili Rama,nilikukatalia nikijua nitateseka...
(Ramadhani na Matatizo ya Ukewenza,DDC Mlimani Park,1986).Wakati Kimulimuli wakiimba kwa tune ya ukali kumuonya binti aache uhuni,Wanasikinde waliimba kwa malalamiko wakimuwakilisha mke aliyekuwa akimlalamikia mumewe.

Kwa ufupi watunzi wa zamani kwa ujumla wao walikuwa na akili sana.Akili zile zingekuwepo leo,wala kusingekuwa na tabu yoyote kupata nyimbo bomba mno za kombe la dunia Afrika Kusini mwaka huu zinazotafutwa kwa gharama kubwa lakini naamini hakuna utakaoufikia kwa ubora wimbo wa Moro Jazz chini ya Mbaraka Mwinshehe wa kuitakia heri FAT na wachezaji wa timu ya Taifa mwaka 1972,miaka 38 nyuma.

Nani anadanganya watu leo kwamba muziki wa dansi ni muziki wa wazee? Akiingoza Bendi kubwa kama Moro Jazz kwenda kwenye maonyesho ya kimataifa ya viwanda na biashara nchi Japan mwaka 1970,Mbaraka Mwinshehe alikuwa na umri wa miaka 26 tu,umri mdogo kuliko wa Wanabongo flavour wengi.Zahir Ally naye alipotunga wimbo maarufu wa Christina(kitu mapenzi kilianza zamani)akiwa kiongozi wa Kimulimuli Jazz,alikuwa na umri wa miaka 23 tu!

Jabali la Muziki,Marijani Rajabu aliimbia bendi ya STC Jazz akitunga nyimbo kama "Mwanangu Shida" na "Unakwenda wapi ewe mwana" akiwa kidato cha tatu Tambaza Sekondari mwaka 1972 akiwa na umri wa miaka 17 tu! Wote hao watatu waliimba na walikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga vyombo.Kwa hiyo muziki wa dansi siyo wa wazee kama inavyojaribu kushawishiwa sasa.

Kwa leo 2010,ingemaanisha bendi kubwa ya muziki ya Tanzania ingekwenda Osaka,Japan kuliwakilisha Taifa katika maonyesho ya kimataifa ikiongozwa na kijana aliyezaliwa mwaka 1984 anayetunga nyimbo na anayepiga solo kwa umahiri mkubwa mpaka kuitwa "soloist national"! Vilevile,leo hii bendi kubwa kama Kimulimuli ingeongozwa na kijana aliyezaliwa mwaka 1987 na kijana huyo kutunga wimbo ulioibeba bendi huku akiwa na ujuzi kamili wa kupiga magitaa! Na pia STC Jazz ya 2010 ingekuwa na mwimbaji na mtunzi mahiri anayeweza kupiga vyombo vingi vya muziki aliyezaliwa mwaka 1993!

Napenda sana irudi Tanzania ilee ambapo taasisi za umma zilichangia sana kuwepo kwa bendi kubwa za muziki kama za majeshi na za mashirika ya umma pamoja na timu kali za soka kama Pilsner,Ndovu,Sigara,Reli,Tumbaku,Pamba,RTC na kadhalika.Mashirika hayo ya umma pia yalikuwa na timu imara mno za netiboli kama Bima,Bora na nyingine.Timu hizi zilitengeneza wachezaji bora sana kwa manufaa ya Taifa na zilileta ushindani mkubwa kwenye ligi zetu za soka na netiboli na kuzifanya ligi hizo ziwe na msisimko wa hali ya juu zilipopambana zenyewe kwa zenyewe na nyingine zisizo za taasisi za umma.

Kwenye soka kulikuwa na vipaji vingi vya hali ya juu ambavyo vilionekana katika mashindano ya vilabu na ya mikoa(Taifa Cup)yaliyokuwa na msisimko sana kutokana na wachezaji wake kupikwa toka mashindano ya shule za msingi(UMISHUMTA)na ya Sekondari (UMISSETA)yaliyowapika wachezaji wa michezo yote na si soka tu.Matunda ya michezo hiyo ya shule ni kupata wanariadha wengi wazuri waliotuletea medali nyingi kwenye michezo ya kimataifa.

Wakati huo michezo ilikuwa na majukwaa mengi kama hayo ya UMISHUMTA na UMISSETA pamoja na michezo ya majeshi,michezo ya mashirika ya umma,Nje Cup,Mkonge Cup,Taifa Cup na ligi za kandanda.Naupenda wakati huo kwani Watanzania waliipenda kwa dhati timu yao ya Taifa bila kujali wachezaji wake walitoka timu zipi au walitoka sehemu gani ya Muungano tofauti na sasa ambapo mashabiki wengi wa timu ya Taifa wamemezwa sana na uyanga na usimba.

Napenda irudi Tanzania ilee iliyokuwa na redio ya umma(RTD) iliyojaa vitu vya kuelimisha na kusisimua kama fasihi iliyotumika kwenye "Mazungumzo Baada Ya Habari" na vidokezo kabla na baada ya taarifa za habari kama "Chungua uchumi wao,hawawezi kuishi kama sisi..." na kadhalika.Kutokana na wingi wa bendi za muziki,redio yetu hii ilikuwa na kipindi kizuri cha nyimbo mpya cha "Misakato" na kilikuwa na kipindi cha shamrashamra cha "Klabu Raha Leo Show" ambapo kwenye sikukuu tulipata "Iddi Show","Krismasi Show" na "Pasaka Show".

Napenda sana irudi Tanzania ilee iliyokuwa na wasomi wa kweli na siyo magumashi,mafisadi wa elimu.Tanzania ile ilikuwa na wasomi wa kweli kwa sababu kila mwanafunzi alitamani kuyamudu masomo huku kukiwa na waalimu halisi wenye vigezo vilivyokamilika vya kazi hiyo na waliumia kwa kutofikia malengo! Huo ni wakati ambao Watanzania walikuwa wanasoma soma sana vitabu vingi vilivyokuwepo wakati huo.Leo mtu anadanganya watu kwamba unaweza kusoma mambo mbalimbali kwenye mtandao.Inapatikana vipi Tanzania nzima? Je unaweza kutembea nayo kila uendako kama unavyoweza kutembea na kitabu? Tusipotoshe watu jamani,kusoma vitabu bado ni muhimu tu.Narudi pale pale,mbona walioanza kutumia mitandao miaka mingi wanasoma vitabu?

Jamani,ningekuwa na uwezo ningeifanya Tanzania hii iliyolala usingizi fofofo kwenye mambo mengi,iamke na kurudia uchangamfu wake ule wa zamani.Uwezo huo sina na sijui nani anaweza.Yapi katika hayo nawe mwenzangu ume ya-miss sana?

No comments:

Post a Comment