Na Ibrahim Mkamba
"TWIGA Stars oyee! Oyee! Soka ya wanawake zii! Zii!". Maneno haya ya kihisia ya kushangilia yanaweza kutumika kueleza kwa ufupi hali halisi inayohusu ushindi mkubwa na mzuri wa ugenini wa timu yetu ya taifa ya soka ya wanawake,Twiga Stars wa magoli 3-1 na kisha sare ya muhimu ya 1-1 ya hapa nyumbanii dhidi ya timu kali ya wnawake ya Ethiopia na hivyo kusonga mbele mashindanoni kwa jumla ya magoli 4-2 licha ya kuwepo kwa mwamko mdogo na mbaya wa mchezo wa soka ya wanawake nchini.Ushindi wa timu yetu ya taifa ya wanawake ni "oyee" kwani ni mkubwa na mzuri lakini mwamko wa soka ya wanawake nchini ni "zii" kwani ni mdogo na mbaya!
Naomba nitumie fursa hii kwa kuwapongeza sana wachezaji wetu wote wa Twiga Stars kwa kujitolea kwa nguvu zote kutupa raha Watanzania na kulinda heshima ya Taifa letu.Nawatakia heri na fanaka katika hatua ya mapambano inayofuata dhidi ya Elitrea.Naomba lengo letu liwe siyo tu kufika fainali za mashindano haya nchini Afrika Kusini bali angalau kufika kwenye mechi yenyewe ya fainali kabisa ya fainali hizo na tukifikia hatua hiyo,basi mahesabu yetu yawe kubeba kabisa kombe hilo.
Napenda nitumie fursa hii pia kuwapongeza viongozi wa timu hiyo kina Lina Mhando kwa kupangilia mambo vizuri na kuwezesha mafanikio haya.Pongezi nyingi ziwaendee makocha wa timu hiyo kina Charles "Master" Boniface Mkwasa na Mohammed "Adolf" Rishard kwani kutokana na nitakayozungumza leo hapa chini,kazi yao ni kubwa mno kuwafundisha dada zetu kuliko kuwafundisha watoto wa kiume kwenye mchezo wa soka.
Kutokana na kukosa mfumo uliokamilika wa mchezo huo,ni wazi dada zetu hawa wanakutana na kocha wa uhakika wa mchezo huo ndani ya timu ya Taifa tu na ndiyo maana kina Mkwasa na Adolf wanapaswa wafundishe hata jinsi ya kutuliza mpira na jinsi ya kupiga mpira wa kutoa pasi na kadhalika kama nilivyowahi kumuona kwenye picha ya gazetini Adolf akimfundisha dada yetu mmoja wa Twiga Stars jinsi ya kupiga mpira wa lengo fulani.Hongera sana kwa wadau wote waliofanikisha ushindi wa Twiga Stars.
Si mara chache kwenye safu hii nimekuwa nikihoji kuhusu mipango yetu mingi isiyo mizuri ya michezo na ninasikitika safari hii tena nitafanya hivyo kuhusu mipango isyo mizuri ya maendeleo ya soka yetu ya wanawake ambayo kwa sasa ina hadhi kubwa dunia nzima.Naomba nirudie tena na tena na labda kuna siku nitaeleweka kwamba soka ya vijana wa chini ya miaka 20,17 na chini ya hapo itatengenezwa tu na serikali yenyewe na wala si klabu za soka.Kusema kuwa klabu inaweza kutengeneza timu ya watoto wa chini ya miaka 17 ni uongo dhahiri na hata anayeelekeza hivyo anajua kuwa hilo haliwezekani.
Nahoji kama nilivyotangulia mara kadhaa kuhoji kuwa utamuwekaje mtoto wa miaka 15,16 au 17 katika maisha ya soka ya wakati wote wakati mtoto huyo anapaswa awe shuleni sekondari wakati huo huku elimu yetu ya msingi sasa ikiwa mpaka kidato cha nne? Kwa hoja hiyo,ninasisitiza tena kuwa soka ya vijana ya uhakika haitakuwepo nchini mpaka serikali itakapoanzisha shule bora zilizokamilika kivifaa vya kufundishia za michezo za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha sita kwa kila kanda ambamo watoto wetu wenye vipaji vya michezo,ikiwemo soka ya wanaume na wanawake, watasoma humo wakifundishwa na waalimu bora wa masomo yote pamoja na waalimu bora wa michezo. Shule hizo zitakuwa ndizo timu za uhakika za watoto wa umri wa chini ya miaka 17 na 20 wa kiume na kike ikizingatiwa kuwa hakuna mtoto wa kuishia darasa la saba sasa kwani, kama nilivyotangulia kusema,elimu ya msingi sasa ni ya kidato cha nne.Vinginevyo,ni usanii mtupu kutengeneza timu ya uhakika ya watoto.
Ni katika muktadha huo,naona ipo haja pia kwa serikali kuweka mkono katika maendeleo ya soka ya wanawake. Tuna timu nzuri ya soka ya taifa ya wanawake lakini tuna klabu ngapi nchini za soka za wanawake? Hizo chache ziko wapi nchini? Sumbawanga kuna ngapi? Maswa ziko ngapi? Je kuna timu hizo Kibondo na Mahenge? Je si kweli kwamba kote huko kuna timu za soka za wanaume? Je si kweli kwamba hata huko wako wanawake wanaopenda na wanaoweza kucheza soka lakini hawajafunguliwa mlango wa kuingia ndani na kuucheza mchezo huo?
Bila kuwa na klabu za kutosha za soka ya wanawake,tunategemea timu hii ya taifa inayoundwa na kina Esther Chabruma kwa miaka kadhaa sasa itaendeleaje kuwa na uimara ule ule kwa miaka kadhaa ijayo? Kwa msingi huo,ni ushauri wangu kuwa serikali yetu ifanye yafuatayo:- Kwanza,ihakikishe inarudisha haraka sana michezo mashuleni na hivyo kurudisha mashindano ya UMISSETA.Na katika kufanya hivyo,ielekezwe kuwa michezo hiyo mashuleni ijumuishe soka ya wanawake.Katika utekelezaji mzuri wa hilo,ni vizuri ikaundwa wizara ya kisekta itakayojumuisha wizara zinazohusika na michezo na elimu.Pili,serikali itengeneze nyaraka za maagizo kwa ofisi zake za mikoa zenye maafisa utamaduni na michezo za kuweka mkakati wa kiserikali wa kuanzishwa na/au kuimarishwa kwa soka ya wanawake kwenye wilaya zote nchini.
Kwa hilo,serikali kuu inapaswa itoe mwongozo tu wa nini kifanyike huku kila mkoa ukipimwa kwa ubunifu wake wa kufanikisha vizuri suala hilo kama ni kupitia kwa wafanya biashara wakubwa wapenda soka wa maeneo husika,kama ni kwa taasisi za umma zilizopo kwenye maeneo husika na kwa njia yoyote halali ya kufanikisha jambo hilo la kheri. Kwa mpango huo,baada ya muda kutakuwa na ligi za kusisimua za kitaifa za soka ya wanawake,kutakuwa pia na Taifa cup ya soka ya wanawake na tutakuwa na timu ya taifa imara ya soka ya wanawake kwa nyakati zote.Sifa mojawapo ya uongozi bora ni ubunifu kama aliokuwa nao hayati Dr.Kleruu kwenye maendeleo ya kilimo,hayati Dr.Lawrence Gama kwenye maendeleo ya michezo na hayati Edward Sokoine kwenye usimamizi makini na madhubuti wa utekelezaji wa kazi ya umma.
Hebu maafisa utamaduni na michezo wa mikoa wapewe kazi.Kwenye u-Dar es Salaam huu wa ligi kuu yetu,kwenye hali hii ya soka yetu kuendeshwa kwa njia huria na kwenye kufa kabisa huku kwa ngoma zetu za asili ambazo mtu akijihusisha nazo sasa anaonekana amepitwa na wakati,mshamba,mchafu na hakusoma, maafisa utamaduni na michezo wa mikoa na wilaya wana kazi gani! Wapewe kazi ya kuratibu uanzishwaji na uimarishwaji wa soka ya wanawake mikoani.
Faida ya kuimarika kwa soka ya wanawake nchini si ya kimichezo tu bali pia ya kijamii na kiafaya.Wasichana watakaojihusisha na mchezo huo wataondoka kabisa katika kufanya mambo yasiyokubalika na jamii ikiwemo kujihusisha na ngono zembe na kuupata ugonjwa wa UKIMWI.Kwa hiyo utaratibu huo utalifanyia taifa jambo kubwa lililojificha kuliko tunaloliangalia na kuliona kwa macho.
Naomba kuwasilisha maoni yangu kwa utekelezaji ili kesho na kesho kutwa tuseme; "Twiga Stars oyee, oyee.Soka ya wanawake oyee,oyeeee!
MWISHO
0713 297085 na 0786 297085
Saturday, 10 April 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment