Search This Blog

Thursday 29 April 2010

HAKUNA MTU MUHIMU KULIKO WOTE POPOTE PALE


Na Ibrahim Mkamba

KWA mujibu wa kamusi ya Kiingereza ya Longman toleo jipya,neno la Kiingereza "indispensable" lina maana ya tafsiri yangu isiyo rasmi ya mtu ambaye au kitu ambacho ni muhimu saaana kiasi cha utekelezaji kutowezekana bila ya kuwepo kwa mtu huyo au kitu hicho.Kwa sababu Kiswahili hakina neno moja la mtu huyo au kitu hicho,naomba nitumie zaidi neno la Kiingereza,"indispensable" kufikisha ujumbe wangu kwa Watanzania wenzangu.

Mtu kujenga picha kwa wengine kwamba yeye ni "indispensable" ni ugonjwa ambao umekuwa ukiathiri sana mipango yetu mingi muhimu.Timu kubwa ya soka ya nchi hii kama Yanga au Simba,ikikabiliwa na ugonjwa huo,uuzaji wa wachezaji nje unakuwa mgumu kwani kutajengeka imani kuwa Jerry Tegete,Mrisho Ngassa,Mussa Hassan Mgosi au Juma Kaseja ni "indispensable" kwenye timu kiasi cha kuuza wachezaji hao kutaathiri mafanikio ya timu.Huu ni upuuzi uliopitiliza kama nitakavyojadili baadaye.

Leo utasema mwanamuziki huyu hawezi kuruhusiwa kuhama bendi hii kwa sababu yeye ni "indispensable"! Kivipi? Kwani mtaalam wa idara anayoshughulikia Tanzania nzima ni yeye tu? Upuuzi mtupu!

Kimsingi,watu ambao wanajiaminisha kwa wengine kwamba wao ni "indispensable" ni wale wenye sifa za ubababishaji,kung'ang'ania nafasi wakati uwezo wao ni wa kuutilia shaka,wenye upeo mdogo sana na wenye akili zilizochoka kiasi kwamba hawawezi kubuni vitu vipya vya kuyafanya mambo yaende.

Watu hawa mara nyingi hupenda sifa zote za utekelezaji mzuri ziwe zao kwamba wao tu ndiyo waliofanikisha mazuri hayo na ikitokea lawama kiutekelezaji,mara zote hufanya juhudi za kuonyesha kwamba wao hawakuhusika kabisa na kosa hilo licha ya ukweli kwamba yote, mafanikio na kuteleza kiutendaji, yanatokea katika ofisi hiyo hiyo huku wao wakiwemo ofisini!

Moja ya athari kubwa,miongoni mwa nyingi za kuwa na watu wanaojiaminisha kuwa "indispensable" kwenye jumuiya yoyote ni kuwafanya wale wenye uwezo mkubwa kiakili kutotumia uwezo wao inavyopaswa kutokana na kubanwa na hao "indispensable" kama itakavyofafanuliwa baadaye.Matokeo ya hali hiyo ni kwa mipango ya maendeleo ya jumuiya hiyo kwenda chini. Mara nyingi hao wenye uwezo huangalia kwa masikitiko mambo yanavyopelekwa ovyo lakini wanachelea kueleza ukweli baada ya huko nyuma kuponea chupuchupu kufukuzwa jumuiyani kwa kurekebisha kosa la "indispensable" kwa nia ya kujenga.

Si mara zote watu hao hujinadi wenyewe kuwa "indispensable" bali mara kadhaa wanyonge miongoni mwetu huwatengenezea hali hiyo ambayo wao huikubali bila kutoa kauli bali kwa vitendo tu.Angalia,Yanga ikifanya vizuri,sifa zote kwa tajiri wao Yussuf Manji lakini ikiteleza,lawama zote kwa Mwenyekiti Iman Madega na safu yake ya uongozi! Simba ikifanya vizuri,sifa kwa "Friends of Simba" tu lakini ikiboronga,lawama kwa uongozi.Hata makocha hupewa ngazi ya kati kwenye yote mawili,mafanikio na kukosekana kwa mafanikio.

Utashangaa kitu kimoja,eti mtu anakuwa nje kiofisi,sehemu ya mbali na ilipo ofisi hiyo,yaani kona nyingine kabisa ya nchi.Mara linajitokeza suala la kutafutiwa ufumbuzi.Atakachofanya "indespensable" huyo ni kurudi ofisini haraka ili ashughulikie suala hilo! Cha kusikitisha,kutokana na upeo wake mdogo,anaweza kufika na kuvuruga mikakati mizuri iliyopangwa na kuanza kufanyiwa kazi na aliowaacha ofisini ambao akili zao zimejaa ubunifu mwingi.

Mambo yakianza kwenda ndivyo sivyo kutokana na muingilio wa kazi wa "indispensable" huyo asiye na chembe ya ubunifu,inabidi wale wenye ubunifu waachiwe waendelee na mipango yao waliyoibuni ya kuondoa kadhia hiyo.Mwisho mambo yanakaa vizuri na kitakachofuata ni kwa "indispensable" huyo kujinadi kwamba bila yeye kurudi toka alikokuwa,mambo yangeharibika vibaya sana,wakati huo ni uongo mtupu!

Na endapo wabunifu hao wangeamua kumsusia na kumuacha afanye vile alivyofikiri kufanya,ambavyo si sahihi kabisa,baadaye mambo yangeharibika, "indispensable" huyu angesema,"unaona, jamaa zangu hawa ovyo kabisa,wameharibu kazi", wakati aliyeharibu ni yeye.

Sifa nyingine kubwa za mtu anayejinadi kwamba ni "indispensable" ni kutafsiri kama kupingwa na kudharauliwa kila ushauri unaopingana na mawazo yake potofu anaopewa wa kuweka sawa mambo! Na mara zote watu hao hawawapendi wale wenye vipaji vilivyowazidi kuhusu shughuli inayohusika kama uwezo wa kiakili,uwezo wa kiushawishi,uwezo wa kifedha na kadhalika.Kwa hiyo,wakiwa kwenye ofisi moja, "indispensable" huyo huwachukia,kuwapakazia mabaya na kuwatenga watu hao huku akiwakumbatia wale wanaomkubalia chochote bila kuhoji uhalali au umantiki wa kitu hicho! Mara zote huwaelezea vizuri sana kwa watu kwamba hao ndiyo wanafaa kiutendaji! Kwa maelezo rahisi,huwachukia wenye akili nyingi na kuwapenda wajingawajinga wanaoramba viatu vyake!

Kwa ufupi,kama tunataka mambo yetu yaende kwa jinsi dunia ya sasa ya Sayansi na Teknolojia inavyoelekeza,lazima tuondoe huo ugonjwa wa kuamini kuwa kuna mtu "indispensable" mahali popote awe kijana au mzee,mwanamke au mwanaume.Katika dunia ya Sayansi na Teknolojia,kila kitu huendeshwa kisayansi.Iwe Sayansi per se,iwe Sayansi ya Jamii au Sayansi ya maendeleo yenye kanuni zake alizoziasisi Mwanafalsafa Karl Marx.

Shughuli yoyote inayoendeshwa kitimu kama timu ya soka,ya Basketball,ya Netball na vikundi vya sanaa pamoja na kazi za ofisini haina mtu aliye "indispensable".Huyu atoke na ashukuriwe kwa mchango wake wa mafanikio,huyu aingie kwa kuleta mbinu mpya na juhudi mpya.Kuna siku naye lazima aondoke kwani kanuni moja kati ya tatu za maendeleo ya kisayansi ya Karl Marx inasema lazima kuwepo kwa Upinzani ndani ya upinzani (negation of the negation).

Kanuni yake ya kwanza ya maendeleo ni kuwepo kwa muungano wa mitazamo tofauti ndani ya jamii husika na kisha muungano huo kuzua mgongano wa mawazo (Unity and Conflict of the opposites).Baada ya hapo ndipo inakuja hiyo kanuni ya pili ya upinzani ndani ya upinzani inayosababisha kuwepo kwa mabadiliko makubwa toka yale ya kimuundo hadi kufikia yale ya kubadilika kabisa kwa chombo husika (Transformation from quantitative changes into qualitative change).

Kwa hiyo,Yanga inapaswa iwe na watu wengi makini wanaopinga kimantiki na kivitendo hali ya klabu yao kubwa na tajiri sana kuendeshwa kadri tajiri mmoja anavyotaka iendeshwe kwa sababu ni yeye tu anayetoa pesa kwa shughuli zote za timu.Lazima uwepo muungano wa watu wenye mitazamo tofauti ndani ya klabu hiyo baina ya wale wanaoamini kuwa kuna "indispensable" kwenye klabu hiyo na wale wanaopinga kuwepo kwa "indispensable" ndani ya klabu yao yenye utajiri mkubwa mno wa mashabiki.

Muungano huo,utazua mgongano utakaosababisha mwisho kabisa klabu hiyo ikabadilika toka mabadiliko ya hapa na pale ya kimuundo hadi kubadilika kabisa kwa umbo lake na sura yake toka kuwa klabu ya "indispensable" mmoja hadi kuwa klabu tajiri inayojiendesha kama taasisi badala ya kumtegemea "indispensable" huyo mmoja.

Timu yoyote ni timu na kila mtu ana mchango wake katika kuipatia mafanikio timu hiyo,iwe ya michezo,ya sanaa,ya taasisi ya umma,ya taasisi binafsi na kadhalika.Ni makosa sana mtu kujinadi au kunadiwa ndani yake kwamba yeye ni "indispensable".Hakuna mtu "indispensable" katika taasisi yoyote.Simba ilikuwa na makipa kama Athumani Mambosasa,Omar Mahadhi,Moses Mkandawire,Mackenzie Ramadhani,Iddi Pazi mpaka Mohammed Mwameja miongoni mwa wengi sana.Nani alikuwa "indispensable" miongoni mwao? Leo hawapo na baadhi wametangulia mbele ya haki, mbona Simba ina uimara ule ule?

Yanga ilikuwa na kina Shariff Shiraz,Mohammed Virani,Abbas Gulamali,Muhsin Hassanali,Vinod Asar na wengine walioibeba sana kifedha kwa nyakati tofauti.Kama miongoni mwao kungekuwa na "indispensable", leo Yanga isingekuwepo.Mbona ipo imara tu? King Michael Enock wa Sikinde na Joseph Lusungu wa Msondo wameshatangulia mbele ya haki.Enzi ya uhai wao wakitumikia bendi hizo, walikuwa zaidi ya waalimu wa muziki.Leo hawapo na hatunao duniani, mbona bendi hizo bado zinadunda? Wangekuwa "indispensable" leo bendi hizo zingekuwepo?

Nawaomba sana Watanzania wenzangu,hasa wale wababaishaji na wasio na lolote la maana kichwani, waache kujinadi kwamba bila wao mambo hayaendi wakati nchi hii ilikuwa na Waziri Mkuu wa utendaji usio wa kawaida,Edward Moringe Sokoine.Amefariki dunia miaka 26 iliyopita lakini Tanzania ipo tu.Tulikuwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye kuwepo kwake kulikuwa ni nguzo ya umoja wetu.Ametutoka miaka zaidi ya 10 iliyopita na umoja wetu uko vilevile.Kama Nyerere na Sokoine hawakuwa "indispensable",wewe mtu wa kawaida kama mimi utakuwaje "indispensable"?

Kwa ufupi ushirikiano wetu wa dhati,kupeana uhuru wa kila mmoja kutoa mawazo yake ya kujenga na kuyaheshimu mawazo hayo huku yale yaliyo bora kuyachukua kwa utekelezaji na kukubali kusahihishwa unapokosea huku ukizingatia umuhimu wa kupokea mawazo mapya ya kimaendeleo ni muungano wa mambo ambao wenyewe tu ndiyo unaweza kuwa "indispensable" kwa mafanikio yetu na wala siyo kuwepo kwa mtu fulani miongoni mwetu.

Mtu anaweza akaondoka na maendeleo yakapatikana zaidi ya wakati alipokuwepo kwani yeye,na hali yake ya kujiona "indispensable", anaweza kuwa ndiyo kikwazo kikubwa cha mafanikio. Wenye uwezo thabiti wa utendaji na wenye akili nzuri,siku zote, huamini kuwa mafanikio hupatikana kwa ushirikiano wa pamoja wa kila mtu ndani ya timu.Watu hawa hawapendi kabisa kuambiwa wao ni "indispensable" na hawataki kuwemo ndani yao mtu anayejinadi au kunadiwa kuwa ni "indispensable".

Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna mtu wa muhimu kuliko wote mahali popote pale bali umuhimu huo unaonadiwa na baadhi yetu ni wa kufikirika tu na unaweza kuwa kinyume cha ukweli wa mambo.

No comments:

Post a Comment