Search This Blog

Saturday 24 April 2010

HILI NDILO JANDO LA KIENYEJI-1

Na Ibrahim Mkamba

1.0: Utangulizi

HAKUNA ubishi kwamba kwa dunia tuliyomo sasa,ni kashfa,ni kosa kubwa,ni ushenzi na ujinga kwa mwanaume wa kizazi hiki wa madhehebu yoyote na wa kabila lolote kutotahiriwa,yaani,kuwa na govi au kwa lahaja fulani kuwa na mkono wa sweta.Kama ni mila,ni mila gani ya kishenzi namna hiyo inayopaswa kuthaminiwa mpaka dunia hii? Kama ni madhehebu,ni madhehebu gani yanayosema kutahiri ni dhambi wakati manabii wote wa Mwenyezi Mungu walitahiriwa tena wakiwa na umri mdogo? Kwa msingi huo,kama ni dhambi basi mwanaume kutokutahiri ndiyo dhambi.

Kwa ufupi ni kwamba mwanaume kutotahiriwa,kwa sasa,ni jambo lisilokubalika kabisa na kwa hiyo ni vizuri tusaidiane kuhamasishana wanaume wote wa Tanzania tutahiriwe.Nakumbuka nilipokuwa Mzumbe Sekondari,tulikuwa tunalala kwenye nyumba moja,Karume namba sita,na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro wa sasa,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Thobias Andengenye,tuliyekuwa naye kidato kimoja cha tano tukisoma masomo ya Historia,Jiografia na Lugha ya Kiingereza (HGL).

Andengenye alianzisha kampeni nzuri ambayo naikumbuka mpaka sasa ya kila siku usiku baada ya Maandalizi ya Jioni (Evening Preparation) kuwashambulia wote waliokuwa hawajatahiriwa ndani ya nyumba yetu hiyo ya Karume namba sita.Tuliungana naye kuwasema sana wenzetu hao bila mlengwa maalum.Cha kufurahisha,tulimaliza kidato cha sita bila kuwemo govi hata moja ndani ya nyumba yetu kutokana na kampeni nzuri ya mwenzetu Andengenye tuliyoshiriki kuiongezea nguvu.

Hivi tujiulize,unakuwaje tajiri sana,maarufu sana kiuongozi,kimichezo au kimuziki na sanaa nyingine kama kucheza filamu huku ukiwa hukutahiriwa? Umaarufu wako una umuhimu gani na govi lako? Kwa sasa,bila kujali mila za baadhi ya makabila yao dhidi ya tohara ya wanaume, hata watoto warembo,kama huyu ambaye sura yake inaonyeshwa upande wa kushoto na umbo lake lote upande wa kulia akitupambia makala hii, hawafurahi kuwa na washikaji wasiotahiriwa na wenye ushujaa na mapenzi ya kweli huwakera washkaji wao wasiotahiriwa warekebishe dosari hiyo.

Makala hii inahusu mila na desturi ya jando miongoni mwa wapogoro,wambunga,wandamba na wangindo wa Wilaya za Kilombero na Ulanga.Nimeona nieleze ninayoyakumbuka kuhusu mila hiyo ili kuwafahamisha wengine na kuitunza kwenye maandishi ikizingatiwa kwamba sasa hivi watoto wetu tunawapeleka kutahiriwa hospitali na miongoni mwa makabila mengi hakuna wanaotahiriwa porini kwa kisu bila ganzi na kuishi huko hadi wapone.Kwa hiyo,taratibu,mila hiyo inatoweka.Naomba tuwe pamoja kufichuliana siri za jandoni,ambalo enzi hizo,lilikuwa kosa kubwa mno.

2.0: Siku ya kutahiriwa

Takriban miaka 40 iliyopita,baba yangu mzazi ambaye kwa sasa ni marehemu,alituita mimi na ndugu zangu na kuomba maoni yetu ya endapo tulipenda tutahiriwe hospitali au kienyeji.Kwa kauli moja tuliamua twende porini kwa kuzingatia jinsi wale walioenda hospitalini walivyokuwa wanachopewa shuleni kwamba wameingia jando hafifu la kukatwa kwa ganzi.

Licha ya baba kupingana nasi akizingatia shuruba alizozikabili mwenyewe kwenye jando hilo la porini na licha ya ukisasa wake uliotokana na usomi wake akiwa Mwalimu wa Shule ya Msingi,sisi hatukubadili msimamo na tulisisitiza kwenda porini.Kwa bahati mama mzazi ambaye naye kwa sasa ni marehemu,alikuwa upande wetu.Baba akashindwa na kuruhusu tufanye kile tulichochagua.Kwa kuzingatia kuwa sisi ni Wapogoro wa Wilaya ya Ulanga,tulipenda twende kwenye jando la mila ya kabila letu ingawa wilayani Kilosa,tulikokuwa tukiishi,majando ya kienyeji ya kabila la Wasagara yalikuwepo.

Shule ya msingi Ulaya,iliyopo kilometa 32 (maili 20) kusini ya mji wa Kilosa ndani ya Wilaya ya Kilosa,Mkoani Morogoro tuliyokuwa tukisoma ambayo baba wetu alikuwa mmoja wa walimu, ikafungwa kama shule nyingine.Tukapanda basi la MORETCO la njia ya Kilosa-Malinyi tukiwa na mama mpaka Ifakara.Safari yetu ikaendelea mpaka kuvuka mto Kilombero kwa pantoni.Huko ng'ambo,ndani ya Wilaya ya Ulanga, tukavuka vijiji vya Kivukoni,Dokoyaya,Mngulungulu hadi Minepa.Hapo ndipo pakawa mwisho wa safari yetu.

Bila kupoteza muda,kila kitu kikawa kimeandaliwa.Alfajiri ya siku iliyofuata,pembe la mnyama lilipulizwa kama tarumbeta kuashiria kwamba shughuli ilikuwa imeiva. Tukaamshwa na kupata uji mzito wa mchele kabla ya kuanza kunyolewa nywele.Mara wengine wakajiunga nasi nao wakaanza kunyolewa nywele.Tukawa jumla ya watoto kama kumi hivi.Kilichofuata,kila mmoja wetu alibebwa begani kuelekea eneo la shughuli yenyewe tukiwa tumefungwa lubega ya kanga kila mmoja wetu bila nguo yoyote zaidi.

Mara nikaona kaka yangu,ambaye kwa sasa ni marehemu, anakimbizwa mbio kuelekea uelekeo fulani baada tu ya filimbi kama hizi za polisi kupulizwa.Mara nikasikia sauti nyingi na kubwa zikiimba: kuulisewa nami ntakwenda kulisewa,kulisewa nami ntakwenda kulisewa... Kila walipoweka pozi ya kuimba ili waanze tena kuimba maneno hayo,nilisikia sauti ya kaka yangu akilia kwa uchungu. Dakika kama tatu au nne baadaye,nikasikia filimbi na mara moja ikawa zamu yangu kukimbizwa kwenda eneo la kutahiria.

Nilipofika hapo,nilikuta kundi kubwa la watu,wengi wakiwa watoto, na mimi nilipelekwa moja kwa moja mpaka kati kati ya kundi hilo.Kanga ikavuliwa kwa nguvu na nikawa uchi kama siku niliyozaliwa.Nilikamatwa na mzee mmoja wa makamo ya kati mwenye nguvu nyingi aliyeibana kwa nguvu miguu na mikono yangu.Nilifanyiwa operesheni kwa kisu ambapo ndani ya dakika kama tatu za uchungu mwingi ,hasa eneo la chini,kila kitu kikawa tayari na niliondolewa kwenda kukalishwa jirani na kaka yangu.Hakuna aliyempa mwenzake pole wala hongera!

Mara moja tukapewa singa zilizotengenezwa kwa vitambaa vya kanga zilizochanwa chanwa kwa ajili ya kujifukuzia nzi.Si zaidi ya nusu saa baadaye,wote tukawa tayari tumekalishwa kwa mstari na vipepeo vyetu vya nzi.Hatua iliyofuata,iliumiza kuliko hata kisu chenyewe! Tuliwekewa pamba zenye spiriti kuzunguka majeraha yote.Uchungu wake ulizidi wa kisu chenyewe!

Baadaye wakaletwa watoto wa marika yetu kutuonyesha sehemu zao za uume na wazee kutuambia kuwa tusiwe na wasiwasi kwani nasi tutakuwa kama wao tukipona. Banda letu likijengwa na likiwa halijakamilika,siku ya kwanza tuliimaliza tukiwa chini ya mikorosho,miguu tukiitanua saa zote.Chakula siku hiyo,tangu wali wa mchana mpaka wali wa jioni hakikulika vizuri na sisi wali wa jando.

3.0: Maisha ya jandoni>
Siku za mwanzo jandoni zinaumiza sana,jeraha la tohara linauma,haja ndogo inatoka kwa maumivu makali na lazima uende kwa tahadhari kubwa ili sehemu hata ndogo ya haja hiyo isiende kwenye jeraha,kulala kwa kufungwa miguu ili uume usiguse sehemu nyingine ya mwili na mengi ya kutesa.Licha ya hali hiyo,ratiba ya siku ilianza kufuatwa mara moja huku msamiati wa jandoni ukisisitizwa mara moja kwa kutumika kwa mazungumzo yote badala ya msamiati wa kawaida.

(a)Ratiba ya siku

(i)Usiku wa saa tisa

Ratiba ya siku sijui ilianzia wapi kwani shughuli zake zilikaribia kuchukua saa 24 zote! Labda nianze pale wali wa jando walipoamshwa kwenye saa tisa usiku.Umepata kausingizi kadogo mara unasikia kama unaota Nyakanga au Mlombu (Kungwi) yeyote yule akiwaamsha kwa kuita "Ohoo" nanyi, miongoni mwa wale ambao walishatoka usingizini, wakiitikia,mara nyingi kwa unyonge sana "Ohoo".Majibizano hayo yalifanywa mara kadhaa kisha huyo Nyakanga au Mlombu alianzisha wimbo wa kuamsha: "Kamwali amka", nanyi mkiwa wote macho sasa mnaitikia, "tuimbe msimu",kisha anaendelea kuimba kwa kusisitiza "amka,amka", nanyi mnaitikia, "tuimbe msimu" kila anavyowaimbisha.

Kinachofuata ni mfululizo wa nyimbo za jandoni zenye mafundisho tupu ambazo mara nyingi zilikuwa zinaunganishwa kama DJ anavyounganisha muziki bila kusimama (nonstop).Kama akiamua kubadaili wimbo,kiashiria chake ni "ohoo!" na wali wa jando kuitikia "ohoo" mara kama mbili hivi katika utaratibu ambao kule JKT hufanywa kwa "Wii!" na kuitikiwa "Waa!".Utaratibu huo wa jandoni hutumika kila shughuli rasmi ya kuimba inapoanzishwa.

Basi usiku huo hapo jandoni mlianza kuimbishwa mfululizo toka "kwelekweche katumbo kana ngwali" mara "Yule kapita pale" mara "ukaya twaweli wanhtu" mara "kulisewa nami ntakwenda" na nyimbo nyingi sana kama hizo ambazo tune yake ilikuwa moja.

Aidha,ziliimbishwa nyimbo zenye mafunzo tupu pia kama "baba kajenga banda karibu na bustani,waarabu toka Unguja banda walitamani",,"madege yale juu ya mkwanga,mkwanga uteluke madege yatue", na nyingi sana zenye tune za aina fulani moja.

(ii) Alfajiri

Kwenye majira ya saa kumi na robo alfajiri,shughuli ya kuimba hufikia tamati na wali wa jando hutolewa nje kwenye baridi kali ya mwezi huo wa Juni kwenda kupiga magoti na kubinua makalio uchi kabisa ili majeraha yapulizwe na ubaridi mkali ikiwa ni tiba mojawapo.Mnakuwa mmebong'oka hivyo,ambapo kwa kipogoro huitwa kufulama huku mkiimba,"tufulame mhmbepu na mtera tufulame" kwa kipogoro ikimaanishwa "tubong'oke baridi na dawa tubong'oke".

Huko "kufulama" huchukua kama nusu saa hivi hadi saa kumi na moja kasorobo mnapoinuka,mnapovaa lubega na kuanza kuliita jua lichomoze mkipiga makofi na kutoa ishara ya kuita upande ambao jua litachomozea huku mkiimba "kajua kwela mmiyombo kwela kwela,kwela mmiyombo kwela kwela". Shughuli hiyo hudumu mpaka jua litakapochomoza saa kumi na mbili na dakika au kasoro dakika chache asubuhi. Na hukamilika mara linapomalizika kutokeza lote.

Kinachofuata kwenye ratiba ya siku ni kupakwa mwilini unga wa mchele uliolowekwa huku mkiimba "kapemba kalawili mashamba twawose tweneli kupakala" wimbo wenye maana ya kuwa unga huo umetoka shambani na wote tuenee kupakaa.Baada ya hapo,chai nzito na uji wa nguvu hufika toka nyumbani kwa wali wa jando mbalimbali na kifungua kinywa hicho hufikishwa bila mbwembwe za kijando jando tofauti na ilivyo kwa chakula cha mchana.

(iii) Asubuhi

Baada ya kupata kifungua kinywa,kama kulikuwa hakuna shughuli yoyote ya dharura kama kuadhibiwa kwa kosa la mmoja,baadhi au wote kwa kosa moja au makosa tofauti,saa za asubuhi zilitumika kufundishwa nyimbo ambapo baada ya muda,"maktaba" ya wali wa jando ilikuwa na nyimbo nyingi mno zilizogawanyika miongoni mwa za kuimbwa popote pale na mbele ya mtu yoyote yule hata nje ya kambi ya jando pamoja na zile zenye maana nzito mno ambazo ilikuwa marufuku kuimbwa nje ya kambi ya jando hata kama ujumbe wake ulikuwa wa mafumbo makubwa yasiyoeleweka.

Nyimbo zenye ujumbe mzito ziligawanyika kati ya hizo za maneno yaliyoficha ujumbe na zile ambazo kila kitu kilitamkwa wazi wazi wazi.Ninapozikumbuka nyimbo hizi za aina ya pili, mpaka leo,ikikaribia miaka 40 tangu niwe porini,mwili wangi unasisimka!

Kwenye majira ya saa tano asubuhi,wali wa jando walianza kuimba wimbo wa kuombea chakula ambao uliimbwa kwa sauti ya juu mno "nikolele mnaze nikamlindi mama,mama njalo katumbo kalegea" na kisha kuendelea na kibwagizo tu cha "mama njalo katumbo kalegea,mama njalo katumbo kalegea".Ujumbe mkuu wa wimbo huu ni kuwajulisha kina mama zetu kwamba njaa ilikuwa inauma na matumbo yalikuwa yamelegea kwa njaa.

Neno "njala", kama ilivyo kwa makabila mengi ya kibantu,lina maana kwa kipogoro "njaa". Wanapoimba "njalo" ni kama wanaweka msisitizo wa kusema "njala o" lakini herufi "a" ya mwisho inaondoka kwenye kutamkwa na kubaki "o" moja kwa moja na hivyo kuwa "njalo".

Wimbo huo ulisitishwa kidogo pale sahani ya wali kutoka kwa mama wa kwanza ilipofika jandoni.Hapo sahani hiyo ilikwenda kupokelewa kwa mletaji kuimba toka huko alikoipokea nje ya eneo la jandoni:- "kiranja mhmbokelage digali dya mbulaga,fumbi mhbokelage digali dyambulaga" na wali wa jando waliitikia "dedede mtwa weto dedede,dedede mtwa weto digali dyambulaga". Vinginevyo,iliitikiwa "dedede mtwa weto dedede mtwa weto,dedede mtwa weto dedede mtwa weto,oo mtwa weto,oo mtwa weto"

Mletaji akishaifikisha sahani hiyo,hujitikisa na kuimba akiuliza,"pakutula nhntuleje" na wali humuitikia "gutuli utetema". Hapo aliuliza kwa kuweka (sahani hiyo) awekeje na wali wa jando kumuitikia aweke ukitetemeka na hapo sahani hiyo ya wali inakuwa imeshapokelewa.Baada ya kuipokea sahani hiyo,wimbo wa kuomba chakula uliendelea na utaratibu ukawa huo huo kwa kila sahani iliyopokelewa mpaka zote kuenea.

(iv) Mchana

Baada ya sahani zote kuenea kwenye majira kama ya saa saba hivi adhuhuri,kiongozi wa Makungwi (Walombu),huanza taratibu za kugawa chakula hicho kwa kuanza kujichotea chake akiimbisha:"natomo natomo njoo unitomolee" na wali wa jando kuitika "natomo natomo njoo ututomolee" na wimbo huo kurudiwa mara kadhaa huku akichota kwa mkono chakula kutoka kila sahani.

Ghafla anaweza "kuwauza" kwa kuimba: "chakula kibaya kapika mama fulani" (akitaja jina la mwali mmoja wa jando). Hapo mwali yoyote asijisahau na kuanza kuitikia "chakula kiba...".Wote mtapata karinye karinye kubwa mno kabla ya kula chakula.Mnachopaswa kujibu ni "mbukwa" basi."Mbukwa" ni neno la jandoni la kutokubali jambo kwa maana ya si la kiadilifu na la kuombea msamaha ama kwa kutamkwa tu au kwa kuimba "mbukwa mbukwa (Mlombu au Nyakanga) wetu mbukwa"

Kinachofuatia ni kula chakula ambapo kikikaribia kwisha,wa mwisho kutahiriwa,aliyeitwa Sungura,alipaswa kuachiwa chakula kidogo kwani yeye alichukuliwa kuwa mdogo na hivyo alikuwa ndiye mtoa vyombo.Baada ya kupona pona kidogo,msipomuachia,hubeba sahani wakati wowote na kukimbia nayo akamalizie kula huko kwingine.Mara nyingi alifukuzwa sana kunyang'anywa sahani hiyo ya chakula.Kuepuka hali hiyo hatarishi kwa wali wa jando,ilikuwa busara kumuachia kwa amani chakula kidogo kwenye sahani.

(v) Alasiri

Baada ya chakula cha mchana kwenye saa nane alasiri kunakuwepo na mapumziko yasiyo rasmi ya saa kama tatu hivi yaliyojumuisha kufundishwa nyimbo na kuelezwa maana zake pamoja na kufundishwa jinsi ya kufanya katika shughuli ya kutembelea nyumbani kwa wali wa jando usiku wa siku kadhaa zinazofuata.

(vi)Jioni

Saa 11 na dakika chache jioni, wali wa jando walianza kuimba wimbo wa kuliaga jua linalozama kwenye saa 12.30 jioni au karibu ya muda huo.Kulikuwa na nyimbo mbili maarufu.Wa kwanza: "sualele sualele kajua kagenda sualele".Maneno hayo yalianzishwa na mwimbishaji na wali wa jando kuitikia,"sualele sualele kajua kagenda sualele".Baadaye mwimbishaji aliendeleza tu kuimbisha hivi na kuweka madoido kadhaa: "Oo kajua kagenda" na wali wa jando wakiitikia hivi kwa muda karibu wote kama mwimbishaji hataanzisha tena ubeti wa kwanza:"sualele kajua kagenda sualele" huku mwimbishaji aki-'rap' kwa maneno "kajua kagenda" na "kagendaaa kajua kagenda"

Wimbo wa pili ambao haukuchangamka sana na ulichosha kuimbwa kwa muda mrefu hivyo uliimbwa ukianzishwa na mwimbishaji; "Sualele wali wangu sualele" na wali wa jando waliitikia;"kajua kagenda" kisha mwimbishaji kuimba; "Fumbi na Kiranja wali wangu sualele" na wali wa jando kuitikia vilevile kisha mwimbishaji huimba; "sualele"na wali wa jando kuitikia "aa aa sualele kajua kagenda"Wimbo uliendelea hivyo hadi jua lilipozama huku katika nyimbo zote hizo,wali wa jando walipiga makofi mara moja moja na kuonyesha ishara ya kulisukuma jua liende au lizame kinyume na ishara ya asubuhi ya kuliita jua lije juu au lichomoze.

Kwenye ratiba ya siku,shughuli hiyo ilifuatiwa nakupakwa unga wa mchele katika utaratibu ule ule wa asubuhi na kwa wimbo ule ule.Kwenye saa moja mpaka saa mbili usiku ni muda wa chakula cha jioni.

(vii) Usiku

Baada ya hapo ni kukaa sehemu za kulala kwa kujilaza na kuimbishwa nyimbo nyingi mpaka kwenye saa 7 usiku ulipoimbwa wimbo wa kuwalaza ulioimbwa "njechembe, njechembe mbati gogo we njegame"na wali kuitikia kwa kuimba maneno hayo hayo kisha kibwagizo kikawa cha maneno hayo hayo.

Saa mbili tu baadaye,mnaamshwa tena kuanza siku mpya na ndiyo maana awali nilisema ilikuwa vigumu kujua ratiba ya siku ilianzia wapi.Kwa kumaliza sehemu hii ya kwanza ya makala hii,naomba nifafanue vitu ambavyo vitaelezwa kwa kina kwenye sehemu inayofuata.Humu ametajwa Kiranja, Fumbi na Fumbi gogo.Hawa ni wa kwanza kutahiriwa (Kiranja),wa pili (Fumbi) na wa tatu (Fumbi gogo).Wengine hawakuwa na majina mpaka wa mwisho aliyeitwa Sungura.

Hili ndilo jando la kienyeji.Naomba tukutane kwenye sehemu ya pili kwa kupeana siri zaidi za jando hilo.

No comments:

Post a Comment