Search This Blog

Thursday, 22 April 2010

HONGERA SIMBA SPORTS CLUB 2009/2010 !


Na Ibrahim Mkamba

BAADA ya kuukosa ubingwa wa Tanzania Bara kwa misimu miwili,yaani 2007/2008 na 2008/2009,Simba Sports Club wamebeba ubingwa huo msimu huu wa 2009/2010 toka mikononi mwa watani wao wa jadi,Yanga,walioushikilia ubingwa huo kwa miaka miwili mfululizo katika misimu iliyotajwa hapo juu.Simba wanastahili pongezi kubwa kwa kubeba ubingwa huo bila ya kupoteza hata mchezo mmoja hadi siku walipofikisha pointi zisizoweza kufikiwa na timu nyingine na hadi walipomaliza kabisa ligi.

Wamecheza mechi 22,wameshinda 20 na kutoka sare mbili dhidi ya Kagera Sugar na African Lyon.Kwa matokeo hayo,kati ya pointi 66 zote,Simba wamepoteza nne tu kwa timu walizotoka nazo sare na hivyo kukusanya jumla ya pointi 62.Walifanya kazi kubwa sana wana Msimbazi hao hasa baada ya kupata sare ya kwanza ugenini Bukoba, nyumbani kwa Kagera Sugar.

Sare hiyo ya 1-1 ilikaribisha vichwani mwa baadhi yetu picha kwamba kuanzia hapo bingwa hakuwa akijulikana baina ya Yanga na Simba na baadhi yetu tukaandika hivyo magazetini! Tena makala au habari zilizokuwa na mwelekeo huo zilikuwa na uzito mkubwa kuliko zile zilizoeleza kwamba kuwashusha chini Simba waliokuwa juu kwa tofauti ya pointi 10 ilikuwa kazi ngumu mno.

Mambo yakawaendea vibaya zaidi wana Msimbazi baada ya sare nyingine ya 1-1 dhidi ya African Lyon.Hapo,tofauti ya pointi nane juu ikawafanya waonekane kupoteza kabisa uwezekano wa kuubeba ubingwa huo, wakati wataalam wa kweli wa soka waliona, walisema na tulisoma wakieleza kwamba timu yenye mwendo wa kutoshindwa tangu mwanzo wa ligi,ni ngumu kukosa pointi mbili ndani ya mechi tatu isipokuwa kwa maajabu ya soka tu.

Kilichosisimua ni kwamba ilifika wakati mawazo ya baadhi yetu yalijilazimisha kuamini na kuwaaminisha wengine kwamba Yanga walikuwa na uwezo wa asilimia zote wa kushinda mechi zote zilizokuwa zimebaki lakini Simba, ambao tangu ligi inaanza mwezi Agosti mwaka jana walikuwa hawajapoteza mechi huku wakishinda nyingi, ndiyo walionekana kuwa na uwezekano wa kufungwa kwenye mechi hizo zilizobaki!

Kama mpenda soka,niliona ni vizuri msimu huu kwa timu nyingine kuchukua ubingwa na si Yanga kwani ingefanya hivyo, ungekuwa msimu wa tatu mfululizo.Kwa nini timu moja itawale namna hiyo mpaka ijisahau? Ningeiombea Yanga ibebe tena ubingwa huo ingawa ni kwa msimu wa tatu mfululizo kama wangeenda na kasi ya Simba tangu mwanzo wa ligi huku timu nyingine zikisuasua.Ningefanya hivyo kwa hoja kwamba aliyestahili ubingwa,aupate tu na hivyo ndivyo Simba walivyostahili kuupata msimu huu kwa kasi waliyoitumia.

Ni wazi kiushabiki,kila shabiki wa timu huiombea mema timu anayoshabikia na huwaombea mabaya mahasimu lakini maombi hayo huwa magumu kutekelezwa kama unayemshabikia alianza kwa kasi ndogo mno huku hasimu akianza kwa kasi kubwa ya kutafuta mafanikio. Hata zile ngonjera za kuomba Simba ibanwe na kushindwa kutangaza ubingwa mpaka wakati wa mechi ya Watani wa Jadi zilitolewa kishabiki kwa kisingizio cha kuongezeka kwa utamu wa mechi hiyo ya watani.

Ngonjera hizo hazikuwa na mantiki yoyote bali zilikuwa za kuomba mabaya tu kwa mahasimu kwani,kwa hoja za kuifanya mechi ya Watani kuwa tamu,ombi hilo lilikuwa kinyume cha mambo.Kama Simba ingekuwa imebakiza pointi moja, mbili au tatu kubeba ubingwa kufikia pambano hilo,ni wazi pambano hilo lisingekuwa na ufundi wowote ule bali lingejaa butua butua zozote ili mradi ushindi upatikane, kukamiana kulikopitiliza,ushirikina wa hali ya juu,kutoaminiana kwa wachezaji kwa wachezaji na kutoaminiana baina ya timu hizo na waamuzi.

Matokeo yoyote ya ushindi kwa moja ya timu hizo,kama huo wa Simba wa 4-3, yangezusha tuhuma za kijinga kwa waamuzi,baadhi ya wachezaji kuadhibiwa na uongozi na hata migogoro mikubwa klabuni ingeanzia hapo.Lakini kwa sababu Simba waliingia kwenye pambano hilo wakiwa mabingwa tayari huku Yanga wakiwa wa pili tayari, mechi hiyo ya Aprili 18, 2010 ilistahili kuwa ya amani kikweli kwa kujaa ufundi mtupu kutokana na uzuri wa makocha wa timu hizo na ubora wa wachezaji wake ingawa hali haikuwa hivyo!

Sasa jiulize kama mechi isiyo ya kumpata bingwa ilikuwa hivyo,huku Yanga wakiwatafuta wahujumu wa mechi hiyo,hali ingekuwaje kama mechi hiyo ingekuwa ya kumpata bingwa?

Binafsi nilifarijika Simba kumaliza ubishi siku walipocheza na Azam na kushinda kwa mabao 2-0 ya Mkenya Mike Barasa.Pamoja na sababu niliyoieleza ya utamu halisi wa mechi ya watani,matokeo hayo yalirudisha afya nzuri kwa mashabiki wa Simba na wa Yanga.Shinikizo la damu na roho kuwa juu viliwakabili sana mashabiki wa Simba muda wote kabla ya siku hiyo na afya za baadhi yao kuathirika huku wale wa Yanga nao wakiwa na tatizo hilo hilo wakisubiri kwa matazamio Simba kuteleza.

Nani kasema kuwa anayesubiri kwa hamu jambo jema ambalo alikuwa halitarajii sana hana shinikizo la damu na roho yake haiwi juu juu? Hujasikia mtu akiomba mgonjwa wake achukuliwe na Mwenyezi Mungu ili watu wapumzike baada ya kumuuguza sana bila matazamio ya mgonjwa huyo kupona? Hujasikia mtu akiomba hukumu itolewe ili ajue kama anafungwa au anaachiwa huru ili nafsi yake ikubali matokeo yoyote yale na iwe huru kutoka kwenye shinikizo kubwa la damu la kuishi kwa matumaini? Kwa hiyo ushindi wa Simba dhidi ya Azam ulitatua matatizo ya kiafya ya mashabiki wa timu zote mbili za Yanga na Simba ambao kuanzia hapo walikuwa katika hali ya kawaida baada ya hali ya kuwa roho juu juu kumalizika.Narudia tena kusema pongezi nyingi kwa Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara kwenye msimu huu.

Simba wamestahili msimu huu kupata mafanikio haya makubwa kutokana na kikosi hicho kutengenezwa vizuri kikijumuisha wachezaji wazuri wa idara zote waliosajiliwa kwa uwiano sahihi badala ya kurundikwa tu.Bahati waliyo nayo watu wa Simba ni kuwa na Kamati ya Usajili iliyo na mawasiliano mazuri na Mwalimu wa timu,Patrick Phiri,Kamati hiyo kujumuisha watu wanaoujua mpira,wenye uwezo wa kifedha na mapenzi ya dhati kwa klabu yao.

Pili,Simba ina kocha mzuri mwenye mahusiano mazuri na wachezaji ambao kutokana na mahusiano mazuri hayo,hawafurahi kabisa kumuangusha kwa kupata matokeo mabaya.Kocha huyo pia anapendwa na uongozi pamoja na Marafiki wa Klabu(Friends of Simba).Hivyo,ubora wa kazi yake ukichangiwa na hoja hizo nyingine,Simba imepata mafanikio haya.

Yanga wamechukua ushindi wa pili na kupata nafasi ya kutuwakilisha kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho mwakani.Wakati msimu unaanza,Yanga walianza kwa maandalizi duni mno huku uongozi wa klabu ukiwa haujui kambi iwe wapi wakisubiri tajiri wao Yussuf Manji aseme naye kuwa kimya kwa muda mrefu huku wakati ukizidi kutaradadi kabla ya kipyanga cha kuanza ligi kuu msimu huu uliomalizika kupulizwa.

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu,uongozi wa klabu ukatangaza kambi hiyo kuwa Mwanza.Wataenda leo,wataenda kesho,leo,kesho....siku zikawa zinazidi kwenda! Ghafla, tajiri akaibuka hewani na kuuliza,"Mwanza,kufanya nini,wakati jengo la klabu limekarabatiwa?".Angesema hivyo mapema basi,matokeo yake siku za maandalizi zikawa chache na ghafla Wanajangwani wanaingia uwanjani dhidi ya African Lyon.Wakalazimisha sare ya 1-1 kwenye pambano walilozidiwa kidogo!

Wakaenda Songea hivyo hivyo tu na kulala 1-0 kwa Majimaji.Wakafika tu Dar,bila kupumzika wakapata sare nyingine ya tia maji tia maji ya 2-2 kwa kuchomoa goli kwa tuta dhidi ya JKT Ruvu kwenye dakika ya mwisho kabisa.Kama Kiggi Makassy angevurunda jukumu zito la kupiga penalti ya dakika hizo ya kuweka mambo sawa,Mzee mzima angelala mechi ya pili mfululizo!

Baadaye,from nowhere akaibuka tajiri wao Manji na kufuturu na wachezaji tu bila viongozi kuwepo hapo Kempisky Kilimanjaro Hotel na kuwaahidi mambo mazuri wakienda kuifunga Mtibwa Sugar Morogoro na wachezaji hao kutimiza vizuri maelekezo hayo kwa kwenda kuipiga Mtibwa 1-2,Morogoro kwa magoli ya Amir Maftah na Mrisho Ngassa.

Kwa ufupi Yanga wangeweza kuwa chini kuliko pale walipokuwa kwenye msimamo wa ligi kama ligi hii ingekuwa na wapiganaji wengi wa nguvu kama ligi za zamani au kama Azam na African Lyon wangekuwa tayari wazoefu wa ligi kuu hiyo.Hii inatokana na ukweli kwamba timu hiyo kongwe kuliko zote nchini ilikosa mipango ya kisayansi ya maandalizi ya kimsimu kama ya wenzao Simba.

Wakati Simba walikuwa na kocha waliyekuwa na mahusiano naye mazuri,Yanga walikuwa na Dusan Kondic waliyekuwa na vita naye vya maneno vya hapa na pale kuhusu maslahi yake binafsi na mazingira ya kazi.Wakati Simba walifanya scouting ya wachezaji kama Emmanuel Okwi,Umuny,Joseph Owinogera na Stephen Bengo toka Uganda na Hillary Echessa toka Kenya,Yanga walikuwa wakimpokea mtu yeyote aliyedai mchezaji aliyejipeleka Jangwani na ndipo walipowapata kina Robert Jama Mba toka Cameroon, Kabongo Honore na wengine wa nje waliokosa matumizi kwa klabu.

Licha ya kufuatiliwa na kuhitajiwa na Simba,Bengo aliamua kwenda Yanga anayoishabikia kutokana na jinsi anavyomshabikia Edibily Lunyamila aliyekuwa na Yanga iliyobeba ubingwa wa Afrika Mashariki na ya kati mara mbili nchini Uganda (1993 na 1999),Bengo akiwa mdogo akishuhudia vitu vya Lunyamila.

Wakati Simba walipanga kuwa kambi zao zitakuwa Hoteli ya Lamada na Zanzibar kwa msimu wote na kuanza kambi hizo mara moja wakiwa na karibu wachezaji wote,Yanga walikuwa hawajui kama wangekuwa Mwanza au hapo hapo maskani kwao Jangwani,huku wachezaji wakianza kwa migomo ya mazoezi kwa kucheleweshewa mishahara kwa Watanzania na kugomea kuishi klabuni kwa wageni! Katika hali kama hiyo ilibidi ushindi wao wa kwanza kwenye ligi ulazimishwe kwa motisha,jambo ambalo binafsi naliona ni la hatari mno.Vipi wachezaji wakishinda mfululizo bila kupata chochote,si wanaweza kuanza mfululizo wa kupoteza mechi ili wabembelezwe kushinda tena kwa ahadi ya motisha fulani?

Kwa mipango yake,Yanga ishukuru sana kuwa na timu mbovu za ligi kuu, vinginevyo pengo la pointi 13 toka kwao hadi bingwa lingejazwa na Pamba,Coastal Union,Prisons,Sigara na Mtibwa enzi zile tulipokuwa na timu za kikweli za ligi kuu.Hata hao Simba, pointi zote kasoro nne wangezitoa wapi wakati huo? Yanga msimu ujao inapaswa ibadilike,pesa hainunui kila kitu kama hamtapanga mambo yenu sawa sawa kwa mipango ya muda mrefu,angalau ya msimu mzima wa ligi.

Azam wanastahili pongezi kubwa mno kwa kuchukua nafasi ya tatu kwenye msimu wake wa kwanza tu wa ligi kuu huku nafasi mbili za kwanza zikiwa za Yanga na Simba.Kwa jinsi timu hiyo ilivyo na mipango mizuri, ikiwa na timu ya uhakika sana ya watoto,naamini mwakani itafanya makubwa zaidi.Naitakia heri.

Mtibwa ya msimu huu ambayo ni ya nne si ile inayojulikana kwa soka yake inayoifunika Simba na Yanga.Mechi ya mwisho wamefungwa na Simba 0-4,Morogoro.Sikushangaa.Kwanza,Mtibwa hii iliyotoa pointi zote 12 kwa Yanga na Simba na kufungwa jumla ya magoli 12-3 na timu hizo,7-1 Simba na 5-2 Yanga,ilionekana wazi kutokuwa serious na ligi kuu ya msimu huu uliomalizika.Dalili zinaonyesha wakali hao wa Manungu,Turiani Morogoro wako njia moja kuwafuata Pamba,CDA,African Sports,Reli na wakali wengine wa enzi hizo kama wenzao Prisons walivyotangulia msimu huu kuifuata njia hiyo!Katika hali kama hii,kwa nini Watanzania wasishabikie timu mbili tu za Yanga na Simba kwani ndizo pekee zenye uhakika wa kudumu?

Pili,baada ya mechi za mwisho kusogezwa mbele,ni wazi timu pekee zilizokuwa zikijiandaa sana zilikuwa zile zilizokuwa zikihitaji kitu fulani,zaidi kubaki ligi kuu kwani wa kwanza na wa pili walishapatikana.Kwa hiyo,inavyoonekana,Mtibwa hawakujiandaa sana kwa mechi ya mwisho wakiona kuwa hawakuwa na mahitaji yoyote makubwa kwenye kumaliza ligi hiyo.Kwa bahati mbaya mechi yao ya mwisho ikawa na timu iliyojiandaa sana kupambana na Lengthens ya Zimbabwe,Yanga na Haras El-Hadood ya Misri,sasa ulitegemea nini hapo?

Kwa uzuri wa timu zao na uzoefu wao kwenye ligi kuu,JKT Ruvu iliyomaliza ya tano na Kagera Sugar ya saba hazikustahili nafasi ilizokuwemo.Hizi zilipaswa kuwa miongoni mwa timu za kugombea nafasi mbili za juu.Tatizo lao ni kuona wapinzani pekee wa kupigana nao kwa nguvu ni Yanga na Simba tu,jambo lililosababisha walioshuka daraja msimu huu wakumbwe na dhahama hiyo.Kwa kutafuta uzoefu kwenye msimu wa kwanza nafasi ya sita kwa African Lyon si mbaya hasa walipowatupa chini wazoefu kadhaa wa ligi kuu.Naamini mwakani watakuwa bora zaidi na wataingia mashindanoni kusaka ubingwa wa ligi kuu.

Mambo ya Majimaji yalikuwa hayaeleweki msimu huu.Fukuza fukuza yao ya kitoto kwa wachezaji bila ushahidi ndiyo imewaweka kwenye nafsi ya nane,mbili tu kufikia kushuka daraja.Unafungwa na Simba au Yanga,unasema wachezaji wamehujumu,hivi hizo Yanga na Simba unazionaje? Nani hakufungwa na Yanga na Simba msimu huu? Timu zote zimefungwa na miamba hao wa soka wanaoongeza ukali wao kwa uwakilishi wa kimataifa.Unafukuzaje wachezaji kwa kufungwa na miamba hiyo na usimlaumu yeyote kwa kufungwa nyumbani Songea na Toto Afrika,iliyofika huko saa chache kabla ya mechi na Moro United iliyokwishshuka daraja? Ugonjwa ni ule ule,watu wanaingia ligi kuu kwa kuzikamia Yanga na Simba tu.

Toto Afrika wameponea chupuchupu kushuka daraja.Kama Yanga wasingesawazisha bao dhidi ya Prisons kule Mbeya,wastani wake wa magoli ambao ungekuwa -9 ungewabakiza Prisons ligi kuu na Toto Afrika kushuka daraja kwa wastani wa -12 kwani zote zingekuwa na pointi 23.Tatizo la Toto wana akili ya ki-toto.Siku zote mawazo yao ni kusaidiana na Yanga.Hayo mawazo ni ya kizamani.Kitakachowapumbaza sasa ni Yanga kusawazisha bao dhidi ya Prisons na wao kubaki wakiamini kuwa hao Yanga ni "kaka" zao wa kweli waliomuua mtu kuwaokoa! Je Manyema Rangers wangeshinda Tanga dhidi ya Azam waliotoka nao suluhu,Yanga wangekuwa wamewasaidia nini? Je wenyewe Toto wangefungwa au kutoka sare na Kagera Sugar kwenye mechi ya mwisho,Yanga wangekuwa wamewasaidia nini?

Ninasema hivi nikizingatia mambo mawili.Kwanza,jinsi vijana hao wa Mwanza wanavyopigana kwa nguvu zote dhidi ya Simba,kama nguvu hizo wangekuwa wanazitumia kwa mechi zote, wala wasingetegemea msaada wa Kagera Sugar wa kucheza soka ya chini na kuwawezesha kushinda.Hapa simaanishi kwamba mechi hiyo ilipangwa bali ninamaanisha kwamba Kagera Sugar walicheza kwa ku-relax kwani hawakuwa na mahitaji yoyote ya ushindi wa mechi hiyo.

Pili,walipotoka Songea walikoishinda Majimaji 0-1,waliamini Yanga wangewahurumia kwa kuzingatia nafasi mbaya waliyokuwemo kwenye msimamo wa ligi.Walikuwa nyanya wakisubiri msaada wa "kaka" zao.Walipigwa 6-0 na kama wangeshuka daraja kwa kuzidiwa wastani wa magoli,basi "kaka" zao wangekuwa wamechangia sana kuwashusha!

Manyema Rangers,Prisons na Moro United wameshuka daraja.Kikubwa ni kwamba wasivunje timu,wakapambane na kurudi tena baada ya msimu mmoja kama Manyema Rangers walivyowahi kufanya,kukosa msimu wa 2008/2009 tu na kama Polisi Dodoma walivyofanya kukosa msimu huu tu.

Hii ndiyo ligi kuu ya 2009/2010 ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya Simba kwa kupata pointi nyingi kuliko timu zote,kwa kuwa na mchezaji-Mussa Hassan Mgosi- aliyefunga magoli mengi kuliko yeyote wa timu nyingine(magoli 18),kwa kufunga magoli mengi kuliko timu zote nyingine na kwa kufungwa magoli machache kuliko timu zote nyingine.

WALIVYOMALIZA

P W D L GF GA Pts
1.SIMBA 22 20 2 0 50 12 62
2.yANGA 22 15 4 3 46 18 49
3.AZAM 22 8 9 5 30 23 33
4.MTIBWA 22 9 6 7 24 23 33
5.JKT 22 6 7 9 27 29 25
6 LYON 22 6 7 9 22 24 25
7.KAGERA 22 5 9 8 15 22 24
8.MAJIMAJI 22 6 6 10 14 26 24
9.TOTO 22 6 5 11 25 37 23
10.MANYEMA 22 6 5 11 20 36 23
11.PRISONS 22 5 6 11 19 29 21
12.MORO 22 4 6 12 19 32 18

No comments:

Post a Comment