Search This Blog

Tuesday 6 April 2010

MICHEZO NA SANAA NI SUALA LA KIMFUMO

Na Ibrahim Mkamba


NI ukweli usiopingika kwamba mafanikio ya kimichezo ya nchi nyingi zilizofanya hivyo yametokana na serikali zenyewe kutia ubani katika mipango thabiti ya kimichezo.Angalia walio juu katika soka hapa Afrika kama Ivory Coast,Ghana na Cameroon,nikiwataja miamba watatu tu,serikali zao mara zote hazichezi mbali na timu zao za Taifa za soka kuhakikisha "wily-nily" wanafanya makubwa katika mashindano yoyote makubwa.


Lakini, viongozi wa serikali wa nchi hizo wanafanya hivyo si kama wanasiasa bali kama watumishi wa umma wenye uzoefu,elimu ya kutosha,mbinu na upendo wa dhati kwa mataifa yao na wanafanya hivyo kamwe,kamwe,kamwe si kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa hata kama wenyewe wanafanya kazi ya siasa."No",si lazima mtumishi wa nafasi ya juu serikalini awe mwanasiasa hata kama alipata madaraka hayo kisiasa siasa.Mara nyingi watumishi wa umma wasio na usiasa usiasa hufanya kazi nzuri sana kama hayati Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine na wengine kadhaa walio hai ambao sioni kama ni vyema kuwataja hapa lakini wengi wetu tunawajua.


Kinyume chake,mtumishi wa umma anayeizimia sana siasa humezwa zaidi na ushabiki wa chama chake kiasi cha kuwaona wananchi wengine wasio kwenye chama chake kama wahaini fulani hivi,wajingawajinga na maadui! Akili yake zaidi hujielekeza kwenye kutafuta sifa za kukinadi chama chake kwamba "mnaona,haya ndiyo matunda ya chama chetu" ili kuonyesha kwamba wasiomo kwenye chama hicho si lolote,si chochote! Huyu anaweza hata kukwamisha jambo jema la kimaendeleo kama jambo hilo litaleta ujiko fulani,unafuu au baraka kwa wananchi wenzake wasio katika chama chake.


Mwanasiasa huyo akishughulikia michezo na sanaa,akili yake itakuwa tu kwenye kuona michezo na sanaa hiyo itasaidia vipi ushindi wa kishindo wa chama chake na si vinginevyo.Kwa msingi huo,maendeleo ya michezo na sanaa nchini ni suala la kimfumo kama taaluma nyingi zitajumuishwa kama wadau halisi wa michezo na sanaa,tofauti na hata mashabiki kama mimi tunavyojiita wadau wakubwa wa michezo na sanaa kama www.spotisana.com ilivyotufanya wote kabisa kuwa wanamichezo na wasanii!


Nadhani,ili tupate maendeleo ya uhakika,iko haja ya mfumo wetu wa kiserikali ukawa na wizara chache mno,kama tano tu ambazo ni Wizara inayohusika na masuala ya uhusiano wa kimataifa,Wizara inayohusika na Usalama wa ndani ya nchi,Wizara inayohusika na majeshi ya Ulinzi, Wizara inayohusika na masuala ya kazi na ajira na Wizara inayohusika na elimu,basi.


Shughuli nyingine kama viwanda, biashara,jinsia,watoto,kilimo,mifugo,miundo mbinu,fedha,habari,mali ya asili,utalii,utamaduni,michezo,sanaa na kadhalika ziwe chini ya Idara za Nchi (State Departments),kwa mfano,Idara ya Nchi ya Utamaduni na Sanaa (Department of State for Culture and Artistic Works) au Idara ya Nchi ya Maendeleo ya Michezo (Department of State for Sports Development) huku masuala ya fedha yakishughulikiwa na Hazina.

Shughuli zote hizi hazihitaji kusimamiwa na wanasiasa bali zinahitaji kuwa chini ya watendaji wakuu waliobobea kiutaaalam na kiuzoefu kwenye shughuli hizo na watakaopata ajira zao kwa michakato sahihi na si uteuzi ambapo wakivurunda, watawajibishwa katika taratibu za kawaida za ajira. Kiutendaji,hao watawajibika moja kwa moja kwa Rais,Makamu wake au Waziri Mkuu,kutegemeana na mgawanyo wa kazi za wakuu hao watatu wa nchi.Hapo itakuwa ni kazi sana,unafiki au kukomoana hakuna na matokeo yake ni maendeleo tu kwa kwenda mbele!


Zile wizara zitakazobaki,lazima zitajwe kwenye Katiba ili Rais yoyote atakayeingia madarakani azingatie uwepo wa Wizara hizo tu. Mfumo ukiwa hivyo,Idara ya Nchi itakayoshughulika na Maendeleo ya Michezo inapaswa iwe na wana taaluma wafuatao,kwa uchache sana,Wtaalam wa michezo,wachumi,wanasayansi kwa ujumla wake wakiwemo wataalam wa afya,wana-sociology,wanasheria,wahandisi,wanahabari makini,watawala na wataalam wa taaluma ya mawasiliano na hisabati.Hawa wote wakijumuishwa ndani ya Idara hiyo ya nchi,lazima tutafika kwenye fainali za kombe la dunia na kina Filbert Bayi wapya wa kumwaga tutawapata.



Kwenye Idara ya Nchi ya Utamaduni na Sanaa tunapaswa tuwe na watu waliobobea kielimu katika nyanja tofauti za utamaduni kama maigizo na filamu,uchoraji na uandishi makini wa vitabu (fasihi na kadhalika),pamoja na wachumi,wana-sociology,waalimu,wanasheria,watawala na wataalam wa taaluma ya mawasiliano na hisabati.Tukiwapata hawa ndani ya Idara hiyo,muziki wa dansi utarudi juu,uchoraji wa katuni utapata hadhi inayostahili na kwa maneno machache,nchi yetu itapata pato kubwa la fedha za kigeni kwa kuuza sana filamu makini,muziki wa hali ya juu,pamoja na kazi nyingi za sanaa nje ya nchi


Nini mchango wa kila taaluma hizo kwa Idara hizo mbili ni mazungumzo mapya na ya urefu wa kutosha,tutakuwa nayo siku nyingine.Leo tujadili hoja hii.Karibuni.

No comments:

Post a Comment