Search This Blog

Friday, 9 April 2010

TAALUMA NYINGI NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA MICHEZO NA SANAA

Na Ibrahim Mkamba


KOSA kubwa tunalolifanya katika mipango yetu ya maendeleo ya michezo na sanaa ni kuamini kuwa taaluma fulani fulani si muhimu katika mipango hiyo muhimu. Kutokana na kutolitambua kosa hilo na hivyo kutolirekebisha,maendeleo yetu ya michezo yamekuwa ni ya kusuasaua mno huku shughuli za sanaa zikifanywa kuwa huria kwa asilimia zote na hivyo kila mhusika kwenda kivyake!


Ni vizuri tuwekane sawa kwamba taaluma za hisabati,mawasiliano (Information Technology) .sayansi,udaktari,ualimu,uhandisi,sheria na uchumi inasaidia sana kuendeleza michezo ikiunganishwa na taaluma za moja kwa moja za kimichezo kama uongozi na ualimu wa michezo.


Kwa upande mwingine,ukiondoa taaluma za sayansi,udaktari,uhandisi,uongozi na ualimu wa michezo,taaluma zilizobaki zinasaidia maendeleo ya sanaa zikijumuishwa na zile hasa za sanaa kama fasihi na kadhalika. Hii inaonekana kama haieleweki sana.Hebu tuanze kuangalia kwa ufupi taaluma moja moja tukizihusisha na maendeleo ya michezo.  • Hisabati

Wataalam wa hisabati ni mwisho wa matatizo yote katika kupangilia mambo yoyote ya kimaendeleo ila kwa bahati mbaya sana jamii nyingi haziujui ukweli huo na hivyo kutowatumia wataalam hawa, wenye taaluma isiyo ya kawaida, katika kupanga mipango sahihi ya maendeleo.Hawa wana ujuzi wa kukuambia kwamba kama unahitaji kufanikiwa katika jambo fulani unapaswa uanze na nini mpaka wakati gani,halafu simamisha hiki kwa muda huu na anzisha hiki.Hiki cha pili kikifikia hatua hii,anza kutekeleza kile cha kwanza pamoja na hiki.Viwili hivi vikifikia hatua hii,simamisha kabisa na anza lile kubwa lao ambalo likifikia hatua hii,yale mawili yaunganishwe nalo na hapo utapata mafanikio haya na haya.


Wataalam hawa wakitumika vizuri,watashauri kwa usahihi sana mipango yetu ya soka, kwa mfano, ipangiliwe pangiliwe vipi kwa kuhusisha shule za soka,soka ya vijana,soka ya kulipwa nje ya nchi,uwepo wa walimu bora wa soka,uwepo wa ligi madhubuti za soka,uwepo wa viongozi makini wa soka na uwepo wa kanuni nzuri na za kutekelezeka za soka.Kipi kitangulizwe na kiende mpaka wapi ndipo kianze kingine na vipi viende kwa pamoja na kwa muda gani kabla ya tathmini ya kwanza.Watu wa hisabati tu ndiyo wanaweza kukupangia kisayansi mambo hayo kwa kutafuta maendeleo. Tuwatumie hivyo baadhi yao badala ya wote kuwaacha kuwa waalimu wa vyuo vya elimu ya juu tu.  • Mawasiliano (Information Technology)

Watu wa taaluma hii ndiyo watunzaji wa uhakika, kwa njia ya elektroniki, wa kumbukumbu zote za mipango yote ya kimichezo ambapo siku za usoni ukitaka kujua kiliazimiwa nini cha kimichezo na kingepatikana kwa njia ipi,hawa jamaa watakupa kumbukumbu zote hizo.Mtu atasema kuwa hilo linaweza kufanywa na mtu wa taaluma yoyote ile.Hapana.Kwanza,hata kama linaweza kufanywa na mtu wa taaluma yoyote,lakini wa taaluma hii atalifanya kwa uhakika zaidi.Pili,jamaa hawa wana uwezo wa kutengeneza programu mbalimbali za kompyuta, rasmi kwa kufanikisha mipango kadhaa mizuri ya kimichezo,jambo ambalo mtu asiye wa taaluma hii haliwezi.Wasiachwe pembeni wataalam hawa kwenye mipango yetu ya maendeleo ya michezo.  • Sayansi

Mwanasayansi per se ni muhimu sana katika maendeleo yetu ya michezo kwani ni yeye ndiye atakayeshauri aina ya vyakula vya wachezaji na viliwe kwa mpangilio gani kutegemeana na aina ya michezo. Ni yeye atakayeshauri saa za wachezaji kulala. Kwa ujumla wote ataaangalia mambo yote ya kiafya ya wachezaji kabla hawajaumia au kuumwa. Ni muhimu sana wanataaluma hii kutumika katika kutafuta maendeleo yetu ya michezo.  • Udaktari

Umuhimu wa wanataaluma wa taaluma hii kwenye maendeleo ya michezo hauhitaji maelezo marefu kwani kila mtu wa michezo anaufahamu. Wao huangalia afya za wachezaji wanapoumia au kuumwa. Mchezaji majeruhi hachezi bila daktari kuthibitisha kwamba anaweza kufanya hivyo.Wana umuhimu mkubwa mno madaktari kwenye michezo yote.  • Ualimu

Ni kosa kubwa kuwaacha nje wenye taaluma ya ualimu katika maendeleo ya michezo.Kwa jinsi taaluma yao ilivyo,waalimu ni walezi na wanasaikolojia.Ukiwaweka nje wanataaluma hawa, ni wazi utaweza kusababisha baadhi ya wanamichezo kuuchukia na kuuacha mchezo walio na kipaji nao kikubwa kwa sababu ya kero fulani fulani zinazowasababisha wafanye mambo ya kuwafanya waonekane washenzi mbele ya wenzao kwenye timu.Wasio na taaluma ya ualimu,huwatimua wachezaji hao kwamba hawana nidhamu lakini kumbe wangewekwa kwanza mikononi mwa walezi wenye uelewa wa saikolojia,matatizo yao yangebainika na wangewekwa kwenye mstari mzuri kimaadili na kuendelea kutesa sana kwenye michezo kwa faida yao na ya taifa lao. Walimu ni muhimu sana kwenye maendeleo ya michezo.  • Uhandisi

Hakuna maendeleo ya michezo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa shule maalum za michezo,viwanja rasmi vya michezo na miundombinu ya kufikia kwenye shule hizo na viwanja hivyo. Ni wenye taaluma ya uhandisi wa ujenzi (civil engineering) tu ndiyo wenye uwezo wa kushauri kuhusu vitu hivyo vya muhimu.Yaani shule ya michezo iwe na vitu gani na wao ndiyo wanaojua viwanja rasmi vya michezo mbalimbali viweje.Wahandisi wasiachwe nje kwenye maendeleo ya michezo.  • Uanasheria

Nemo judex in causa sua, delegatus non potest delegare,in pari delicto portior est conditio defendentis,audi alteram partem,actus non facit reum nisi mens sit rea. Hii ni misemo michache ya kilatini inayotumika sana katika shughuli za kisheria.Msemo wa kwanza unamaanisha "mtu hapaswi kuwa jaji kwenye kesi inayomhusu".Msemo wa pili unamaanisha "aliyekaimishwa madaraka hapaswi kuyakaimisha kwa mwingine".Unaofuatia unamaanisha "kwenye utata kiushahidi,utata huo lazima umnufaishe aliyeshtakiwa".Halafu ule mwingine una maana "sikiliza pande zote kwenye kesi" na wa mwisho unamaanisha "kitendo hakimfanyi mtu kuwa mhalifu wa kosa kama hakuwa na nia ya kutenda kosa hilo".


Misemo hiyo inaonyesha jinsi taaluma ya sheria ilivyojaa busara tele na mantiki kibao! Wenye taaluma hii ni muhimu sana kwenye maendeleo yetu ya michezo kwani ni wao ambao watatengeneza kanuni zenye mantiki na za kutekelezeka na ni wao ambao watakuwa washauri wazuri katika kuepuka kufanya mambo ya kutuletea hasara kikanuni. Ni wachambuzi wazuri wa mambo mbalimbali ya kimaisha.Ni muhimu sana kuwajumuisha kwenye mikakati ya maendeleo kimichezo.  • Uchumi

Ikizingatiwa kuwa michezo inaweza kuingiza pesa na kuwatajirisha wahusika fulani wa michezo hiyo kama klabu za soka na chama cha soka cha nchi,watu wenye taaluma ya uchumi ni muhimu sana katika mipango yetu ya maendeleo ya michezo.Ni muhimu sana kwao kujumuishwa kwenye mipango yetu.


Huu ndiyo mchango wa taaluma tofauti katika maendeleo yetu ya michezo.Tunapopanga chochote cha kimaendeleo kimichezo,tufikirie haja ya kuwajumuisha wenye taaluma tofauti kama ilivyoelezwa hapa.Mara nyingine tutaangalia mchango wa taaluma tofauti kwenye sanaa.No comments:

Post a Comment